Akizungumza na Chama cha Wanawake Wakatoliki
Tanzania (WAWATA) hivi karibuni, Askofu Pengo alitoa wito kwa waumini kuachwa
huru wafanye maamuzi yao wenyewe juu ya kuipigia kura ya ndiyo au hapana Katiba
Inayopendekezwa badala la kushinikizwa na viongozi wa dini kuipigia kura ya
‘hapana’ katiba hiyo.
Aidha, amesema kamwe hawezi kubadili kile
alichosema kwani ni ukweli anaouamini na alishaweka hilo wazi.
Askofu Pengo alisema hayo jana wakati wa ibada
Maalumu ya Shirikisho la Kwaya Katoliki (Shikwaka ) iliyofanyika katika Kanisa
Katoliki Kipawa, jijini Dar es Salaam ambako kwaya zaidi ya 100
zilishiriki.
“Jana (juzi) baada ya ibada kule Kurasini
walikuja waandishi wa habari na tukaanza kujadiliana na baadaye nilipomaliza
wengine kisirisiri walijadili kwa nini sikusema chochote kuhusu Katiba
Inayopendekezwa; Sasa ndugu zangu niseme mara ngapi,” alihoji.
“ Hivi ni nani anaweza kufikiria naweza kubadili
maneno niliyosema, leo niseme kweli na kesho hapana. Nitakuwa mtu wa aina gani
wa kubadili maneno na misimamo,”alisema.
Alifafanua kuwa alishasema ukweli anaoujua hivyo
hana sababu ya kuurudia na kwamba kufanya hivyo ni kutafuta ugomvi. ‘’Yale
niliyosema kuhusu suala hilo nimesema mara moja na ni mara moja tu basi,’’
alisisitiza.
Askofu Pengo aliwataka waamini na wasio waamini
waliomsikia na kukubaliana na aliyosema, kuwa ni wakati wao kuendeleza taarifa
hiyo kwa kusambaza katika sehemu mbalimbali.
Akirejea habari za kufufuka kwa Yesu, alisema
kusambaza msimamo wake kutaenea kwa watu wengi zaidi kwani ndivyo injili ya
ufufuko wa Bwana Yesu ilivyoenea kwa Petro ambaye awali wakati wa mateso ya
Yesu, alimkana lakini mara baada ya kufufuka alisambaza taarifa hizo.
Askofu Pengo alisema mashemasi kama
Filipo,Stephano na wengine hawakumwachia Petro kusambaza ufufuko wa Bwana Yesu
ila kila walipokwenda walitamka kuhusu ufufuko na hakukuwa na haja ya kumuita
Petro kuelezea ufufuko huo.
Alisema wasingefanya hivyo injili isingefika
duniani kote .
“Hivyo hivyo wale walioamini niliyosema kuhusu
msimamo wangu wa Katiba Inayopendekezwa, waendelee kusambaza kila wanapokwenda
kwa manufaa ya nchi,” alisisitiza.
Alisema ndivyo inayofundishwa na fumbo la ufufuko
wake Yesu kwa jambo jema halitegemei mtu mmoja kurudia rudia kwani atakera watu
kutokana na kuwapo wanaosikia jambo moja mara kwa mara.
Askofu Pengo alisema anapoongelea tamko lake
kuhusu Katiba si kwamba anataka kugeuza nafasi ya ibada kuwa mahali pa
kutangaza siasa au shughuli za kijamii, bali neno lolote analofanya ni ukweli
wake na hatobadili.
Alitaka waumini kusimama na kusema potelea mbali
katika kusimamia ukweli wa kile wanachoamini kwa kuwa jasiri bila kuogopa
chochote na kuwa sawa na mtu anayesema liwalo liwe.
Pengo alisema katika ulimwengu wa sasa, umuhimu
wa kutamka ukweli na liwalo liwe, unazidi kudhihirika kutokana na madai ya
nyakati kwani ni muhimu kwa maaskofu, mapadre na hata viongozi wa serikali kila
mmoja ana nafasi ya kutamka ukweli.
Ugaidi
Aidha, Pengo alizungumzia tukio la ugaidi nchini
Kenya lililosababisha vifo vya watu zaidi ya 147 na kusema hakuna aliyefikiria
kuwa Kenya inaweza siku moja kuzingirwa na watu na kufanyika mauaji yenye
msimamo wa imani za dini.
Alisema ingawa nchi hiyo ilikuwa na malumbano
kadhaa, lakini si dini. Alisema tukio hilo halipendezi si kwa Waislamu wala
Wakristo.
“Tumuombe Kristo atuponye na kutuepusha na balaa
hilo, na yasiendelee kutokea kwa jirani zetu huku kila mmoja akihakikisha kuwa
na ujasiri wa kubaki na msimamo wetu,’’ alisema.
Waraka wa maaskofu Mwezi uliopita Askofu Pengo
wakati akifungua Mafungo ya WAWATA, yaliyofanyika Kanisa Kuu la Mtakatifu
Joseph, Dar es Salaam alikosoa waraka wa maaskofu kupitia Jukwaa la Kikristo,
uliotaka waumini kupiga kura ya hapana kwa Katiba Inayopendekezwa.
Alisema kuwaamulia ni kuwadharau kuwa hawana
uwezo wa kufanya maamuzi sahihi wao wenyewe na kuingilia uamuzi wao.
Awali, Jukwaa la Wakristo Tanzania liliwataka
waumini wake kujiandikisha kwa wingi katika Daftari la Kudumu la Wapigakura,
kuisoma Katiba Inayopendekezwa na kujitokeza kuikataa kwa kupiga kura ya
“hapana”.
Taarifa hiyo ilisainiwa na Mwenyekiti wa Jumuiya
ya Kikristo Tanzania (CCT), Askofu Dk Alex Malasusa, Mwenyekiti wa Baraza la
Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa na Mwenyekiti
wa Kanisa la Pentekoste Tanzania (CPCT), Askofu Daniel Awet.
Waliompinga Pengo
Baada ya Askofu Pengo kutoa msimamo wake, Askofu
wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima alimkashifu na kumtuhumu
kusaliti viongozi wenzake wa Kikristo, kitendo kilichosababisha kukamatwa na
kuhojiwa na polisi.
Chanzo: Habari Leo
No comments:
Post a Comment