Wakazi wa Kibamba Mjimpya, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam wakiwa wamefurika nyumbani kwa Emmanuel Joseph (32), ambaye ni baba wa mtoto aliyedaiwa kufariki dunia mwezi Agosti, mwaka jana. |
Wakazi wa Kibamba Mjimpya, nje kidogo ya Jiji la Dar es
Salaam jana walifurika nyumbani kwa Emmanuel Joseph (32), kushuhudia maajabu ya
tukio la kufufuka kwa mtoto aliyedaiwa kufariki dunia mwezi Agosti, mwaka jana.
Mtoto huyo mwenye umri wa mwaka mmoja nusu (jina linahifadhiwa),
inadaiwa alizikwa katika makaburi ya Mlongazila.
Anadaiwa kufariki Agosti 7, mwaka jana baada ya kuugua
ghafla na kuishiwa damu.
Mtoto huyo anadaiwa kurudishwa akiwa hai na Juma
Nakochinya (33) maarufu kwa jina la Bino, mkazi wa eneo la Pandambili mkoani
Dodoma ambaye hutibu kwa njia ya maombi.
MAMA MZAZI AFUNGUKA
Akisimulia tukio hilo, mama wa mtoto huyo, Hellena Mtoro (23) , alisema ilikuwa
siku ya Jumamosi majira ya saa 11:00 jioni ambapo mwanawe akiwa na umri wa
miezi tisa alizidiwa ghafla na kumkimbiza hospitali ya Mbezi kwa matibabu.
Alisema baada ya kufika hospitalini hapo, vipimo
vilionyesha ameishiwa damu hivyo alihamishiwa hospitali ya Tumbi, iliyopo
Kibaha mkoani Pwani.
“Madaktari walijitahidi kadiri ya uwezo wao kutafuta
mishipa ya damu maeneo tofauti ya mwili ikiwamo kichwani, cha ajabu mishipa
ilikuwa ikionekana lakini ilikuwa inavimba, wakati madaktari wakihangaika,
ilipofika saa 6:00 usiku alifariki dunia,” alisema.
Hellena alisema taratibu zote za maziko zilifanyika na walimzika
kwenye makaburi ya Mlongazila yaliyopo karibu na eneo analoishi.
Alisema baada ya kuzika siku tatu baadaye walielekea
Dodoma kwa ajili ya kumaliza msiba na kurudi Dar es Salaam.
“Ukweli ni kwamba kifo cha mtoto wangu kilikuwa sio cha
kawaida, hivyo tulianza maombi na mume wangu, tulikuwa tunasali kwa Nabii Flora
Peter, ambaye baada ya kumweleza mazingira ya kifo hiki, alimuweka kwenye
maombi na kututaka tumpelekee picha yake,” alisema na kuongeza:
“Baada ya maombi alitueleza kuwa anamuona mtoto wetu yupo
hai na anaamini atarudi siku moja. Tuliendelea na maombi na siku moja
nilikutana na mama Mariamu ambaye baada ya kumwelezea kifo cha mtoto wangu,
aliniambia kuna kijana anaitwa Bino ambaye anaweza kumrudisha kama alikufa
kichawi,” alisema.
Alisema mama huyo alimpa namba ya mtu huyo na
alipowasiliana naye, Bino alimtaka ashike Sh. 100.
“Nilifanya hivyo na baada ya dakika tano tukiwa bado
hewani, alinijulisha kuwa mtoto wangu anamuona yupo hai hivyo akanitaka niende
kesho yake Dodoma kwa ajili ya kukamilisha kazi hiyo ya kumrudisha,” alisema.
Hellena alisema siku iliyofuata alisafiri kuelekea Dodoma
na aliwasili saa 10:00 jioni ambapo alienda moja kwa moja kwa mganga huyo.
“Saa 1:00 jioni Bino alichukua mwiko, ungo na kinu, vifaa
anavyovitumia kwenye kazi yake. Ungo aliuweka chini na akaanza kusoma dua kisha
nikamuona mtoto amekaa ndani ya ungo ule, nilishtuka sana baada ya kumwona
akiwa hana hata nguo, amechafuka na aliyechoka,” alisema.
Alisema baada ya tukio hilo, mtoto alibaki kwa mganga
huyo kwa ajili ya kuendelea na matibabu zaidi.
Alisema alikaa kwa mganga huyo kwa muda wa siku mbili na
kurudi Dar es Salaam na kumuacha mtoto huko kama alivyotakiwa.
“Jana (juzi)
aliletwa na Bino ili aje kutusalimia kwa kweli nashukuru Mungu kwa
sababu hali ya mwanangu inaendelea vizuri, afya yake ipo vizuri, ” alisema.
Alipoulizwa kama anaamini tukio zima la kurudishwa kwa
mtoto wake, Hellena alisema yeye ni Mkristo na kabla ya kwenda huyo alianzia
kanisani na maono yalionekana yupo hai.
Aliongeza kuwa, anaamini kilichofanyika ni kutoka kwa
Mungu kwa sababu mtu huyo hatumii matunguri zaidi ya kumuomba Mungu kisha
kufanya kazi zake.
BABA: HII NI MIUJIZA
Baba wa mtoto huyo, Joseph, alisema kuwa tukio hilo ni la
kwanza na la aina yake kwenye ukoo wao na kwamba lilipotokea hakuna aliyeamini
hadi walipomuona mtoto.
Alisema baada ya mtoto wake kuletwa, majirani ambao
walishiriki kwenye msiba wake, walishtuka na kujaa nyumbani kwake kitendo
ambacho kiliwalazimu kwenda polisi kutoa taarifa ya kile kilichotokea.
Alisema baada ya kufika Kituo cha Polisi cha Mbezi kwa
Luis, walihojiwa pamoja na Bino na baadaye kuruhusiwa kurudi nyumbani.
BINO ANENA
Nakochinya maarufu kama Bino alisema kuwa, tukio la
kuwarudisha watu wakiwamo watoto kwenye ulimwengu wa kawaida, sio la kwanza.
Alisema kuwa miongoni mwa watoto aliowarudisha na
kuwakabidhi kwa wazazi wao idadi yao kwenye mabano ni pamoja na Mtongani
Kunduchi (1), Mtwara (2), Mbagala (1), Masasi (1) na Nachingwea (1).
Alisema ana mwaka mmoja toka aanze kazi hiyo na anaifanya
kwa kutumia maombi.
Alisema idadi ya aliowasaidia ni zaidi ya watu 150
wakiwamo watoto na vijana na kwamba baadhi yao bado anaendelea kuishi nao kwa
matibabu zaidi.
“Mtu anapokuja kwangu kama alivyofanya huyu mama, mizimu
ikikubali nitoe huduma mhusika hutakiwa kutaja majina yake na huyo aliyefariki
kisha huwa namtaka atoe Sh. 100 ambayo huitumia kumwangalia aliyekufa alipo,
anapoonekana aliyefuata huduma yangu hutakiwa kutoa Sh. 30,000 ya mkoba ambayo
ni sadaka,” alisema.
Alisema mtoto huyo bado yupo mikononi mwake kwa matibabu
zaidi, atakapomaliza atamkabidhi rasmi kwa wazazi wake.
JIRANI
Alfonce Eneliko alisema kuwa, alishiriki kwenye msiba wa
mtoto na ameshtuka baada ya kumuona kwenye nyumba hiyo tena.
“Jana (juzi) jioni niliporudi kutoka kwenye shughuli
zangu nilisikia mtaani watu wakiongelea kuhusu tukio hili la mtoto, nilipofika
hapa kweli nikamuona na aliniambia haya ni maajabu ya Musa, mtoto hajabadilika
sura zaidi ya kukua, “ alisema.
Aidha, NIPASHE ilizungumza na msichana mmoja
aliyejitambulisha kama Jennifer Mwenda (23), mwenyeji wa Njombe, ambaye alisema
aliambatana na Bino kumleta mtoto huyo kwa wazazi wake, kuwa naye alisimuliwa
kuwa alifariki dunia akiwa na ujauzito na kurudi kwenye uhai baada ya kuombewa
na kijana huyo.
Jennifer alisema nyumbani kwa Bino wanaishi ndani na wale
waliopona hutoka na kutembea mitaani hata dukani.
Mjumbe wa nyumba kumi Michael Yuso, alisema kuwa bado
hajapokea taarifa rasmi za tukio hilo zaidi ya kumshuhudia mtoto huyo jana.
“Kweli nimemuona na cha ajabu mwaka jana mimi ndiye niliyeshughulikia
eneo la kuzikwa na alizikwa kweli, lakini hichi kilichotokea ni kitendawili
naendelea kufuatilia zaidi,” alisema.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Agustino
Senga, alithibitisha jeshi hilo kupokea taarifa za mtoto huyo na kueleza kuwa,
hatua za awali za kiuchunguzi zinaendelea ikiwa ni pamoja na kujiridhisha kama
alizikwa kweli, alitibiwa hospitali gani hadi umauti ulipomkuta.
Pia alisema wanafuatilia kujua kama kweli wazazi hao wana
cheti cha kifo cha mtoto huyo ndipo hatua nyingine zitakapoendelea.
WENGINE WAVUTIKA
Mmoja wa wanaume waliokuwepo nyumbani hapo ambaye
hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema kuwa, anafanya utaratibu wa
kwenda kwa mganga huyo kumwangalia mtoto wake ambaye alifariki miezi kadhaa
iliyopita kwa kifo cha utata.
“Uchawi upo vifo vingine havitokani na kusudi la Mungu,
ndugu zetu wanapotea katika mazingira kama haya lakini kwa sababu hatuna wa
kutusaidia basi wanabaki wakiteseka huko walipo, mwanangu alikufa katika
mazingira yasiyopishana na huyu, nataka kujiridhisha,” alisema.
No comments:
Post a Comment