Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limemtaka Mkuu wa Kanisa
la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima, kuhamisha makazi ya kanisa lake
lililopo katika viwanja vya Tanganyika
Packers, Kawe, jijini Dar es Salaam leo.
Meneja Uhusiano wa NHC,
Yahya Charahani alilieleza
NIPASHE kuwa, walimpatia notisi Askofu Gwajima ya kuhama eneo hilo mwezi mmoja
uliopita, lakini hakutekeleza badala yake ameendelea kulitumia eneo hilo
kuendesha shughuli za kanisa lake, zikiwamo ibada.
Charahani alisema eneo hilo ni mali ya NHC na ni maalum
kwa ajili ya ujenzi wa mji wa kisasa na wakazi waliokuwa wanaoishi eneo hilo
walishalipwa fidia muda mrefu uliopita ili kuondoka.
“Lile eneo ni la NHC kwa muda mrefu na kabla ya hapo
kulikuwa na nyumba nyingi sana na zilibomolewa, hizo zilizobaki zimebaki tu
kimakosa,” alisema Charahani.
Aliongeza kuwa, hiyo siyo mara ya kwanza kwa NHC kumpatia notisi Askofu kiongozi huyo
kulihamisha kanisa lake.
Kwa mujibu wa Charahani,
NHC walimpatia notisi Askofu Gwajima ya mwezi mmoja kuondoka katika
makazi hayo na kwamba notisi hiyo ilimalizika Machi 9, mwaka huu.
Alisema baada ya kumalizika kwa notisi hiyo, NHC
lilimpatia muda zaidi Askofu huyo ambao unamalizika leo.
Juhusi za kumpata Askofu Gwajima kuthibitisha kama
amepokea notisi hiyo zilishindikana kutoka na simu yake ya mkononi kutopatikana
kila alipopigiwa tangu Alhamisi iliyopita.
Hata hivyo, jana alipotafutwa Mwanasheria wa Askofu
Gwajima, Paul Mallya kuelezea hatua ya NHC ya kumpa mteja wake notisi ya
kuhamisha makao ya kanisa lake, alisema bado hajapata notisi hiyo.
“Sijapata taarifa hiyo, ndiyo kwanza nasikia kwako, ngoja
nifuatilie nije nikupe majibu yaliyokamilika,” alisema Mallya.
No comments:
Post a Comment