ASKOFU Josephat Gwajima wa Kanisa la Ufufuo na
Uzima, amesema yeye si tajiri kama inavyodhaniwa, bali alichonacho ikiwa ni
pamoja na nyumba, magari na helikopta ni baraka tu za Mungu, lakini kama ni
utajiri, anatarajia siku moja utamshukia.
Aliyasema hayo jana wakati akihubiri kanisani
kwake Kawe,
Dar es Salaam, ambako alisema anawashangaa watu wanaomfuatilia
maisha yake huku wakisema yeye ni tajiri mkubwa.
“Wanaodai mimi ni tajiri wana wivu tu na
wananionea, mimi si tajiri, bali ni masikini kama walivyo masikini wengine.
Natarajia kutajirika hapo baadaye waumini wangu wakiwa matajiri, siwezi
kutajirika kama waumini wangu bado ni masikini, nitatajirika pamoja nao,”
alisema Gwajima.
Kuhusu mgogoro unaoendelea baina yake na Jeshi
la Polisi, Askofu Gwajima alisema yeye anauona kama ni vita vya kiroho na hivyo
ataendelea kumwomba Mungu ili amsaidie kupambana na kilichopo mbele yake na
anaamini kuwa atashinda vita hiyo kwa uweza wa Mungu anayemtegemea.
“Mungu wangu na awasamehe wote wanaonituhumu
kuwa mimi ni tajiri na kuamua kudhoofisha huduma, nasema huduma yangu haitakufa
kamwe na wala hatutayumba katika mipango yetu ya kuhubiri injili. Tutapigana
kwa uweza wa Mungu na tutashinda kama alivyosema kuwa tutapigana pamoja naye na
tutashinda,” alisema Gwajima.
Akizungumzia afya yake, Askofu Gwajima alisema
kwa sasa anaendelea vizuri na anaweza kusimama na kutembea, kuhubiri kama
ilivyokuwa hapo awali na hatarajii kurejea tena kwenye kiti cha baiskeli ya
magurudumu matatu bali atasimama imara daima.
Kuhusu kupeleka nyaraka kadhaa anazotakiwa
aziwasilishe polisi siku ya mahojiano Aprili 16, mwaka huu, Askofu Gwajima
alisema suala hilo bado wanasheria wake wanalishughulikia na wataendelea
kufuata taratibu zote zinazotakiwa na jeshi hilo.
Gwajima anatakiwa kuwasilisha nyaraka muhimu za
hati ya usajili wa kanisa lake, namba ya usajili wa kanisa, hati ya umiliki wa
helikopta, hati ya nyumba anazomiliki, idadi ya makanisa yaliyopo chini yake
pamoja na hesabu za fedha za kanisani kwake zinazohusu mapato na
matumizi.
Nyaraka zingine ni majina ya Bodi ya Udhamini wa
kanisa, mpiga picha za video kanisani kwake siku ya ibada na shughuli zingine
za kanisani hapo pamoja na waraka wa Maaskofu uliosomwa makanisani ambao
Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo alioupinga na kusababisha yeye kumkashifu
kiongozi mwenzake huyo wa dini.
Akionekana kuwa makini sana na lugha anayotumia
wakati wa kuhubiri, Gwajima aliwaomba waumini wake waendelee kufuatilia kila
sehemu na kuchunguza mambo yote mabaya yanayosemwa juu yake na kanisa lake na
kuyaripoti kwake au kwa uongozi wa kanisa ili wayafanyie kazi mara moja kabla
hayajaleta madhara.
“Nawaombeni sana mfuatilie kila chanzo cha
habari na kuchunguza mambo yote yanayosemwa juu yangu au kuhusu kanisa na kuyaleta
mara moja hapa kanisani ili tuyafanyie kazi kabla hayajaleta madhara makubwa,”
alisema Gwajima.
Aliongeza kuwa, “tuendelee kuwa na umoja katika
kipindi hiki ambapo shetani anataka kupigana nasi ili tuweze kushinda.
Tukifarakana hatutaweza bali tukiwa kitu kimoja tutasonga mbele na kuwa
huru”.
Utajiri wake
Wakati akikana kuwa tajiri, mwanzoni mwa mwaka
jana alifanya mahojiano na gazeti hili na kukiri Mungu anambariki, ndiyo maana
mambo yake yanamnyookea.
Aliyasema hayo alipokuwa anazungumzia mpango
wake wa kununua helikopta kwa ajili ya huduma za injili ndani na nje ya
nchi.
Alikiri kutokana na utajiri anaosema unatokana
na baraka za Mungu, anamiliki jumba la ghorofa nne eneo la Mbezi Beach katika
Manispaa ya Kinondoni.
Pia amewanunulia wachungaji wake 40 magari ya
kutembelea kwa bei tofauti, yakiwemo ya chini ya Sh milioni 10 na mengine ya
zaidi ya Sh milioni 20.
“Ni kweli nimewanunulia magari, unajua moja ya
misingi yangu ya maisha ni kwamba, mimi siwezi kuishi maisha mazuri, wakati
wachungaji wangu wanadhalilika, nimewanunulia magari karibia 40.
Lakini nina
wachungaji wa ngazi mbalimbali, hawa ni wale wa juu, wengine wachungaji wadogo
wapo zaidi ya 670, hawa ni watenda kazi muhimu na wanatofautiana kwa ngazi zao,
ndio maana kazi ya Mungu inasonga mbele hata nisipokuwepo,” alisema Gwajima.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment