WATU 18 wamekufa papo hapo kwa kuteketea kwa
moto na wengine 11 wamejeruhiwa vibaya kutokana na basi walilokuwa wakisafiria
kugongana na lori aina ya Mitsubishi Fuso, katika kijiji cha Msimba tarafa ya
Mikumi, barabara kuu ya Morogoro – Mbeya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonald
Paulo alisema ajali hiyo ilitokea jana saa mbili asubuhi katika eneo hilo huku
likihusisha basi aina ya Scania lenye namba za usajili T373 DAH na Fuso lenye
namba za usajili T164 BKG.
Alisema chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa basi
la Nganga ambaye alikuwa katika mwendo kasi na kulipita gari lililokuwa mbele
yake bila ya tahadhari na kukutana na lori hilo na kisha kugongana nalo katika
eneo hilo.
Alisema baada ya magari hayo kugongana, ndani ya
buti ya basi kulikuwa kumepakiwa pikipiki ambayo ilikuwa na mafuta na baada ya
kutokea ajali hiyo kulitokea mlipuko wa moto na kusababisha basi hilo pamoja na
lori kuwaka moto.
Kamanda huyo alisema kuwa kutokana na moto huo,
baadhi ya abiria waliokuwepo katika basi hilo walishindwa kujiokoa na hivyo
miili yao kuteketea kabisa na moto huo, wakiwemo madereva wote wa magari
hayo.
Alisema majeruhi 11 wa ajali hiyo wamekimbizwa
katika Hospitali ya Mtakatifu Kizito iliyopo tarafa ya hiyo Mikumi kupatiwa
matibabu huku hali zao akieleza kuwa baadhi yao ni mbaya kutokana na kuungua
vibaya kwa moto.
Kamanda huyo alisema miili ya marehemu hao
imehifadhiwa katika hospitali hiyo ambapo mpaka sasa haijatambulika majina
yake, licha ya madereva wa magari yote kufa.
Hata hivyo, Kamanda huyo alishindwa kutaja
majina ya majeruhi kutokana na baadhi yao kuendelea kupatiwa matibabu kwa ajili
ya kuokoa maisha yao.
Naye Mganga wa Hospitali ya Mtakatifu Kizito
iliyopo Mikumi, Dk Boniventure Buyagabuyaga, alithibitisha kupokea jumla ya
miili ya marehemu 18 ambao walikuwa wameteketea vibaya kwa moto kutokana na
ajali, ambapo alisema tayari imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhiwa maiti
kwa ajili ya kusubiri utambuzi.
Alisema mpaka sasa majeruhi wanaotibiwa katika
hospitali yake wamebaki saba, lakini hali zao bado ni mbaya kutokana na kuungua
moto katika sehemu mbalimbali za miili yao.
Ajali hiyo imekuwa sawa na mwendelezo wa ajali
za mabasi nchini, kwani Alhamisi iliyopita watu 12 walikufa katika ajali
zilizotokea Tanga na Morogoro, huku wengine wanne waliokuwa wakisafiri kwa basi
la Nyehunge wakiaga dunia usiku wa Jumamosi mkoani Dodoma.
Katika ajali iliyotokea mkoani Tanga, katika
kijiji cha Mbweni Mkata, majira ya asubuhi, ilihusisha basi la Kampuni ya Ratco
ya Tanga liligongana uso kwa uso na basi la kampuni ya Ngorika na gari dogo
aina ya Toyota Passo na kusababisha vifo vya watu 10 papo hapo, akiwemo mmiliki
wa gari dogo, Musa Lupatu aliyekuwa Mbunge wa zamani wa Korogwe
Vijijini.
Katika tukio la Morogoro, watu wawili walikufa
na wengine 48 kujeruhiwa katika ajali iliyosababishwa na basi la Happy Nation
lililokuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Mbeya na kupata ajali eneo la
Mikumi.
Aidha, Machi 12, mwaka huu mkoani Iringa, basi
la Majinja Express lilikuwa likitokea Mbeya kwenda Dar es Salaam liligongana na
lori na kisha likaangukiwa na kontena lililosababisha vifo vya watu 43.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment