Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima akihubiri akiwa amekaa katika kiti cha magurudumu kwenye ibada ya Pasaka jana katika viwanja vya Tanganyika Packers Dar es Salaam. |
Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima
jana alihubiri akiwa katika kiti cha magurudumu na kusema hawezi kuwatupa
Mbunge wa Monduli (CCM), Edward Lowassa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod
Slaa kwa kuwa ni marafiki zake wa siku nyingi.
Pia askofu huyo, amewataka waumini wote wa kanisa hilo
kufika katika Kituo Kikuu cha Polisi,
Alhamisi ijayo siku ambayo atakwenda
kukamilisha mahojiano dhidi ya tuhuma za kumtukana Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la
Dar es Salaam, Polycarp Kardinali Pengo.
Akihubiri mamia ya waumini waliofika kanisani hapo kwa
ajili ya ibada ya Pasaka jana, Gwajima alisema kumekuwa uvumi kwamba kuhojiwa
kwake na polisi kulitokana na kuwakaribisha wanasiasa hao kanisani kwake kwa
nyakati tofauti na kuzungumza na waumini wake.
Alisema alifahamiana na Lowassa tangu mwaka 1996 wakati
huo mbunge huyo akiwa Waziri wa Ardhi na tangu kipindi hicho amekuwa mtu wake
wa karibu.
Alisema alifahamiana na Dk Slaa tangu mwaka 1994 kabla
hajagombea nafasi ya urais kupitia Chadema na kwamba tangu wakati huo amekuwa
rafiki wa familia.
“Hawawezi kunichagulia marafiki, hawa ni watu wangu wa
karibu hata kabla hawajawa na ndoto za kugombea urais, nitaendelea kuwa nao
karibu,” alisema.
Asimulia mahojiano
Akizungumzia mahojiano yake na polisi, Gwajima aliwaeleza
waumini wake kwamba mambo mengi aliyohojiwa hayakuhusiana na suala la
kumkashifu Kardinali Pengo.
“Polisi walinihoji mambo mengi binafsi yanayonihusu mimi
na hayakuhusiana kabisa na Pengo, maswali ya Pengo yalikuwa machache sana,”
alisema.
Hata hivyo, Gwajima alisema hana ugomvi na polisi wala
Serikali kwa kuwa amekuwa akitoa ushirikiano kwa vyombo hivyo. Akitoa mfano,
alisema Februari mwaka huu alipeleka barua polisi kueleza anataka kudhamini
kampeni kwa ajili ya kupinga mauaji ya albino kwa kushirikiana na jeshi hilo.
“Niliwaeleza kwamba tungezunguka na polisi mikoa yote
Tanzania na wamenijibu kwamba nipeleke ratiba ya shughuli hiyo ili tuanze,”
alisema.
Alisema pia alidhamini mafunzo ya ulinzi shirikishi kwa
vijana 400 kwa kushirikiana na polisi... “Shughuli hizi zinaonyesha kwamba sina
ugomvi na polisi, bali nimekuwa rafiki kwa kushiriki katika shughuli zenye
masilahi kwa Taifa.”
Waumini hao walikuwa na shauku ya kumwona Gwajima na
walionekana wakisukumana ovyo kila mmoja akitaka kumwona.
Akiwa amevaa suti ya rangi ya kijivu na shati jekundu,
Gwajima aliteremka katika Hammer akishikiliwa na wasaidizi wake na kukalishwa
katika kiti cha magurudumu mawili kilichokuwa kikisukumwa na wasaidizi hao
kuelekea kwenye jukwaa la kanisa hilo.
Baada ya kufika, vikundi vya kwaya viliendelea kuimba na
kucheza nyimbo mbalimbali za kumtukuza Mungu.
Gwajima alizungumza na waumini wake kuanzia saa 5.30 hadi
saa 6.45, akiwaeleza kilichotokea kuanzia siku alipofika polisi kwa mara
kwanza, mahojiano hadi alipotoka hospitali.
Katika mahubiri yake, Gwajima alisema ataendelea kuwaonya
viongozi wa Serikali na wa dini watakaokosea masuala mbalimbali. “Sitajali ni
kiongozi wa aina gani amekosea nitawakemea. Rais akikosea nitamkemea. Waziri
akikosea nitamkemea na viongozi wa dini wakikosea nitaendelea kuwakemea,”
alisema.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment