Kwa muda mrefu habari za uhusiano wa mapenzi baina ya
watu mashuhuri wakiwamo wafanyabiashara na wanamuziki zimekuwa zikitikisa
vichwa vya habari katika mitandao ya kijamii, redio lakini pia hata kwa wapenzi
wa wadau hao.
Hii ni kutokana na uwazi waliouweka wahusika, lakini pia
inatokana na jinsi wanavyoivutia
jamii yao kila wanapotokea mbele za watu na
kwa matendo yao.
Wapo ambao wameshatangaza kufunga ndoa pia wapo waliopo
katika uhusiano kama wachumba ambapo wametangaza kuvalishana pete pia wapo
ambao hawajafikia hatua hizo.
Mwandishi wetu wiki hii ameliangalia kwa kina suala hili
na akatoka na orodha ya couple sita ambazo zimekuwa gumzo miongoni mwa
mashabiki kiasi cha kuunda makundi katika mitandao ya kijamii kwa kipindi cha
miezi mitano iliyopita.
1. Nuh Mziwanda na Shilole
Wote ni wasanii wa muziki wa kizazi kipya na kwa kiasi
fulani muziki wao ni kama unafanana. Mara kwa mara hualikana jukwaani kufanya
kazi pamoja pindi wanapokuwa na muda.
Uhusiano wao ulianza kama utani, watu walikuwa hawaamini
lakini uthibitisho ulikuja kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram.
Huko ndiko Shilole mwenyewe alikiri kwamba wao ni
wapenzi. Kuna mengi yanatokea, wanagombana na kutupiana maneno huku Shilole
mara kwa mara akimpiga mpenzi wake huyo lakini mpaka leo wapo pamoja kama
pacha.
Huku mtaani tena ndiyo shutuma za kwamba Shilole ni
mkubwa kwa Nuh na kwamba kipato ndiyo kinamuweka Nuh kwa Shilole.
2. Vanessa Mdee & Jux
Hawa nao pia wanafanya muziki wa R&B,
wameshirikishana kwenye kazi na huko ndiko inasemekana walikoanzia uhusiano wao
ambao mpaka leo. Hata hivyo, ni Jux pekee aliyewahi kusema bayana kwamba kuna
kitu kati yao.
Hata hivyo, uhusiano unaonekana dhahiri, kila mmoja
humuongelea vyema mwenzake na kila mmoja anafanya kazi nzuri kwa hiyo
wamejikuta wakipeana mashabiki kila mmoja kutokana na umaarufu wake.
Tetesi za mtaani zinasema huku pia kuna tofauti kubwa ya
umri kati ya Vanessa na Jux lakini kingine pia ni kwamba Jux anadaiwa kuwa na
kipato kikubwa kuliko Vanessa.
Kingine ambacho kinaleta minong’ono ni hatua ya Jux
kuamua kummwaga mpenzi wake, Jack Cliff baada ya tuhuma za kushikwa na dawa za
kulevya nchini China na kuamua kutoka na Vanessa.
3. Faraja na Nyalandu
Hapa unamzungumzia wanandoa Waziri wa Maliasili na
Utalii, Lazaro Nyalandu na mrembo aliyeiwakilisha Tanzania katika mashindano ya
urembo ya dunia mwaka 2004, Faraja Kotta uhusiano wa wanandoa hawa umeingia
katika minong’ono baada ya Nyalandu kutuhumiwa kuwa na uhusiano na msanii
mwenye mvuto wa tasnia ya filamu Tanzania, Aunt Ezekiel.
Wengine wakaenda mbali zaidi na kusema kuwa hata ujauzito
aliokuwa nao mwanadada huyo ni wa mheshimiwa huyo.
Kila mtu alisema lake lakini katika ufafanuzi ambao
ulitoka pande zote mbili ni kwamba kama kwa njia moja au nyingine kuliwahi kuwa
na uhusiano kati ya hawa wawili, ulikuwa ni wa kikazi.
4. Zari & Diamond
Kwa sasa couple hii ndiyo gumzo la mjini. Daimiond ambaye
jina leke halisi ni Nasib Abdul ni kijana aliyewahi kuwa muuza mitumba na
ghafla akaitafuta njia ya kutoka kimaisha kupitia muziki. Bahati ikamdondokea
na sasa kijana huyo ametulia kwa mwanamama wa Kiganda anayedaiwa kuwa na
mkwanja mrefu zaidi ukilinganisha na wanawake wengine nchini mwao.
Mara ya kwanza ilionekana kama kuna mradi wanauhangaikia
pamoja, lakini ghafla ikaja kugundulika kwamba ni watu walio katika mapenzi
mazito tena wanaotegemea mtoto hivi karibuni.
Zarina ana watoto watatu tayari ila Diamond bado ni
kijana mdogo kiumri ukilinganisha na mwanamama huyo. Minong’ono inazidi kila
kukicha katika mitandao ya kijamii na mashabiki wa karibu wa mwanamama huyo
hawaamini kama ni mjamzito hali iliyosabisha kuamua kupiga picha tumbo lake na
kuweka katika mtandao wa Instagramu.
5. Ray Kigosi na Chuchu Hans
Kati ya uhusiano ambao ulipokelewa kwa hisia tofauti
miongoni mwa mashabiki wa tasnia ya filamu ni huu, maana hakuna aliyewategemea
kabisa.
Awali Ray alikuwa na uhusiano Mainda ambaye alikuwa ni
muigizaji mwinzie kabla mwanadada huyo kumpindua na kushika usukani hadi leo.
Inasemekana walikutana katika kazi lakini baada ya kuwa
pamoja, kwa jinsi wanavyojiweka kila mtu amevutiwa maana kila mmoja ameonekana
kuwa na hamu mapenzi aliyonayo kwa mwenzie yasiishe.
Ray Kigosi yeye ni mwigizaji wa tangu awali lakini Chuchu
ni mwanamitindo aliyewahi kushiriki shindano la Miss Tanzania akitokea jijini
Tanga.
Baada ya kuwashangaa kwa muda, kwa sasa kila mtu
anaongelea uhusiano wa hawa wawili unavyozidi kuwa na mvuto kadri siku
zinavyozidi kwernda mbele.
6. Reginald Mengi na Jackline Ntuyabaliwe
Mji unazizima kwa sasa baada ya ndoa ya mmiliki wa
Makampuni ya IPP, Reginald Mengi na mrembo aliyeiwakilisha nchi katika
mashindano ya urembo ya kimataifa ya Miss World 2000, Jackline Mtuyabaliwe.
Wawili hao wamefunga ndoa miezi minne baada ya
kuchumbiana katika sherehe ya kuzaliwa ya mwanadada huyo iliyofanyika nchini
Dubai.
Ukiachana na watoto wao wakiume wawili pacha ambao
walikuwa miongoni mwa wasimamizi wa harusi hiyo, wageni wengine takriban 50
walihudhuria harusi hiyo ambayo ilifanyika katika Visiwa vya Mauritius.
Gumzo lililotawala kuhusu ndoa hii ni kutokana na tofauti
kubwa ya umri na mkwanja mrefu alionao mzee mengi ambao utamsababisha mwanadada
huyu kuungana na mume wake katika kuumiliki kama mwanafamilia na mzazi
mwenzake.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment