Wakati mama mzazi wa msichana anayedaiwa kutaka kujiunga
na Kundi la Al-Shabaab, Tahliya Sadir akisema kuwa anamwachia Mungu suala la
binti yake, babu na bibi yake wameonekana kushtushwa na taarifa hizo na kusema
hawakuwahi kufikiria kama mjukuu wao
angethubutu kufanya uamuzi kama huo.
Akizungumza kwa njia ya simu jana, Tahliya alisema:
“Namwachia Mungu suala hili, siwezi kuchukua hatua zaidi ya hapa.”
Ummul Khayr Sadir Abdulla, alikamatwa Machi 30 katika
mpaka wa Kenya na Somalia, El Wak, Jimbo la Mandera kwa kile kilichodaiwa kutaka
kuingia nchini Somalia ili kujiunga na kundi la kigaidi la Al-Shabaab.
Bibi na babu wa binti huyo, Masoud Salim na Asha Saleh ambao wote ni
walimu walisema hawakufikiria kama jambo hilo lingetokea katika familia yao na
kuongeza kuwa wanaamini ni suala la utoto tu.
“Sisi hii taarifa tumeipata kupitia vyombo vya habari”
aliongea bibi huyo akitokwa machozi.
Bibi huyo alisema
familia nzima ina wasiwasi mkubwa kutokana na ukubwa wa shutuma hiyo
inayomkabili mjukuu wao na hawajui mwisho wake.
Naye, Masoud Salim alisema anaamini kuwa mjukuu wake anajua
anachokifanya kwani mara ya mwisho, aliwaaga anakwenda masomoni Sudan ambako
yeye na dada yake Sumaiya wanasomea fani ya udaktari.
Salim alisema baba na mama yake Ummul- Khayr wako nchini
Kenya kufuatilia suala hilo.
Hata hivyo, Mwananchi lilipozungumza na mama yake Ummul
Khayr, Tahliya alikataa kusema yupo wapi kwa wakati huo.
Ummul-Khayr ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha
Kimataifa cha Afrika, Sudan alikamatwa nchini Kenya akiwa na wenzake wawili
raia wa Kenya, Maryam Said Aboud na Khadija Abubakar Abdulkadir.
Kaimu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, DCI Diwani Athuman
alisema bado wanasubiri majibu kutoka kwa polisi wa Kenya ili kuendelea na
taratibu za kumrudisha msichana huyo nchini.
“Tumeshangaa hatujajibiwa lolote mpaka sasa, lakini
wakitujibu taratibu zote zitafuatwa,” alisema
DCI Diwani.
Ummul-Khayr alimaliza madarasa ya Quran Zanzibar na
baadaye alipata elimu yake ya juu katika Shule ya SOS kabla ya kujiunga na
elimu ya Chuo Kikuu nchini Sudan.
Naibu Kamishna wa Uhamiaji, Abbas Irovya alisema, ofisi
yake imehakiki uraia wa msichana huyo na kujiridhisha kuwa ni Mtanzania.
No comments:
Post a Comment