Makada wawili wa CCM wilayani Bagamoyo, wameonyesha nia ya kuingia kwenye
kinyang’anyiro cha ubunge katika jimbo hilo kupambana na mbunge wa sasa, Dk
Shukuru Kawambwa.
Makada hao ni Mwenyekiti wa CCM kata ya Dunda, Yusufu
Mrisho Kikwete ambaye ni
kitinda mimba wa familia ya Rais Jakaya Kikwete na
Abdursharrif Zahoro ambaye ni mwenyekiti
wa Jumuia ya Wazazi CCM wilayani humo.
Wakati makada hao
wakitangaza nia hiyo juzi, tayari mbunge wa jimbo hilo Dk Shukuru Kawambwa alikwisha tangaza nia ya kutaka kutetea
nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Tambo za wapinzani wa Kawambwa
Abdulsharrif alisema ameamua kuingia katika kinyanganyiro
hicho baada ya makundi mbalimbali ya
wakazi wa wilaya hiyo, wakiwemo kina
mama na vijana kumuomba achukue fomu ili aweze kuwania nafasi hiyo.
“Nimefuatwa sana
jamani na wananchi wa hapa, wakati mwingine hadi naona aibu kujificha maana
nahisi ni Mungu amewaonyesha kiongozi anayewafaa safari ijao, kwa hiyo
nimekubaliana na maombi hayo, nitajitokeza kukabiliana na Dk Kawambwa,”
alisema.
Naye Yusuph Kikwete alisema ana matumaini makubwa ya kushinda kwa kuwa,
amekuwa akiungwa mkono na makundi mbalimbali, wakiwamo vijana ambao wamekuwa
wakimshawishi kugombea nafasi hiyo.
“Ni kweli kuna
makundi mengi, yamekuwa yakinishawishi kuingia katika kinyang’anyiro na baada
ya kutafakari sana na kujipima kama ilivyo kwa wanasiasa wengine, nimeona
siwezi kukataa ushawishi huo, maana kuna watu wameona uwezo wangu wa kiuongozi,” alisema.
Mapema wiki hii Dk
Kawambwa aliweka wazi kuwa anaingia tena katika kinyang’anyiro hicho kutokana
na kuridhishwa na mambo mbalimbali aliyofanya kwa wapigakura wa jimbo hilo.
“Ninarudi na wana Bagamoyo wameniomba nifanye
hivyo kutokana na kufanya mengi ya
maendeleo, mfano katika kipindi changu cha miaka kumi, nimeweza kushughulikia
changamoto kubwa zilizokuwa zikiwakabili wakazi wa jimbo hili, ikiwamo masuala
ya elimu, afya na maji.
“Lakini kubwa, ni kushughulikia matatizo ya ardhi na
malipo ya fidia,” alisema.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment