MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi wilaya ya Shinyanga imemhukumu
kifungo cha maisha jela mkazi wa mtaa wa Kitangili katika manispaa ya Shinyanga
baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka na kumpa ujauzito mtoto wake wa kambo,
mwanafunzi wa darasa la tatu.
Alimbaka mtoto huyo kutimiza masharti ya mganga
ili kutoa tiba kwa mkewe.
Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi
mwandamizi wa wilaya, Thomson Mtani alisema mahakama imeridhika na ushahidi
uliotolewa na upande wa mashitaka ukiongozwa na wakili wa serikali, Judith
Tuka.
Mtuhumiwa Osward Charles (45) mkazi wa Kitangili
alifikishwa mahakamani kwa tuhuma mbili. Kosa la kwanza likiwa ni kumbaka mtoto
wake mwenye umri chini ya miaka kumi ambaye ni mwanafunzi kinyume na kifungu
namba 130, kifungu kidogo cha kwanza na cha pili na kifungu namba 131 kifungu
kidogo cha pili cha sura ya 16 cha kanuni ya adhabu.
Kosa la pili ni kumwingilia kimwili mtoto wake
ambaye ni mwanafunzi wa shule na kumpa ujauzito kinyume na kanuni ya tano ya
sheria ya elimu ya mwaka 2003 inayotoa adhabu kwa watu wanaowaoa na kuwapa
mimba wanafunzi wa shule kama ilivyo katika kifungu cha 35 kifungu kidogo cha
tatu cha sheria ya elimu ya 353.
Ilidaiwa na mwendesha mashtaka mwanasheria wa
serikali Judith Tukakuwa, kati ya Novemba 12 mwaka 2012 na Septemba katika eneo
la mtaa wa Kitangili manispaa ya Shinyanga mshitakiwa alimbaka mtoto wake wa
kambo ambaye ni mwanafunzi mwenye umri wa miaka tisa na kumsababishia
ujauzito.
Awali mshitakiwa katika mwenendo wa kesi alikana
kutenda makosa hayo lakini katika utetezi wake mbele ya mahakama kabla ya
kutolewa kwa hukumu hiyo ili mahakama impunguzie adhabu alikiri kumbaka mtoto
wake mbele ya mama yake mzazi kwenye kitanda kimoja baada ya kupewa maagizo ya
mganga wa jadi kama sehemu ya tiba ya mke wake aliyekuwa akisumbuliwa na
maradhi.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment