....Kisa kinasikitisha hiki, tuache kutumia vitu vyenye ncha kali tunapowaadhibu watoto.
Mtaa wa Mwatulole, wilayani Geita mkoani Geita, ndiko
anakopatikana mtoto Saidi Idd , (so jina lake halisi), mwanafunzi wa darasa la
kwanza katika Shule ya Msingi Mwatulole mwenye umri wa miaka saba.
Ni mtoto anayeishi na wazazi wake lakini
ndiye mtoto
mkubwa kati ya watoto wanne anayetegemewa na wenzake.
Nafika nyumbani kwao nikiongozana na mtoto huyo, walimu
wake na Ofisa wa Polisi Dawati la Jinsia.Tunapokelewa na mwanamke
anayejitambulisha kuwa ni shangazi yake na Saidi.
Tulijitambulisha na kumhoji kama anafahamu jambo lolote
juu ya tukio la ukatili alilofanyiwa mtoto huyo na mama yake mzazi, Mariam
Hassan la kumchoma mkuki eneo la paji la uso na kumsababishia majeraha makubwa.
Mwanamke huyo anakataa kufahamu tukio hilo, kwa madai
kuwa haishi nao isipokuwa alipigiwa simu na Mariam aje amlelee watoto kwani
yeye (Mariam) anakwenda kufungwa.
Mara alituitia mdogo wake Saidi aliyekuwa ndani, alitoka
lakini alionekana kuwa katika hali ya huzuni na aliyedhoofika.
Unyonge wa mtoto huyo uliashiria kuwa kuna jambo zito
kwenye familia hiyo. Alitusalimia kwa adabu huku akijitambulisha kuwa anaitwa
Amina Iddi (si jina lake halisi) mwenye umri wa miaka sita.
Aliingia ndani na kutuletea viti, tukaketi na kuanza
kuzungumza na mtoto huyo, ambaye alionekana kuwa na siri nzito moyoni.
Alitusimulia mkasa wa kaka yake alivyochomwa mkuki Machi
26.
Asha anasema mdogo wake alikuwa anacheza na wenzake nje
ya nyumba yao muda wa jioni, ghafla mama yao alifika na akamuuliza (Asha) alipo
Said.
Anasema alimwita na alichukua mkuki ambao huwa anautunza
ndani kwa ajili ya kuwapigia, akamchoma usoni, akaondoka kwenda kulala kwa
sababu tu kaka yake hakufua nguo za shule.
“Aliondoka kwenda kulala bila hata kumwangalia kaka kama
aliumia. Ila alikuwa anatokwa na damu, nikachukua maji nikamwagilizia ili
kuzuia damu zisitoke na kumfunga nguo usoni. Damu zilikuwa zikimtoka sana,”
anasema Asha na kuongeza:
“Mama aliingia chumbani na kulala, wala hakujali kama
tumekula, tulikwenda kulala baada ya kumfunga kaka nguo, asubuhi tukaamka
kwenda shule wala hakutuaga.”
Anasema wakati wanakwenda shule, kaka yake aliendelea
kutokwa damu baada ya kufungua ile nguo aliyokuwa ameifunga kwenye jeraha.
Anasema yeye na kaka yake wanasoma shule na darasa moja,
wakiwa darasani walikuja walimu wakamwona anatokwa na damu wakamwita ili
awaeleza kilichomsibu kaka yake.
“Niliwaambia kuwa alichomwa mkuki na mama usiku,
wakamwita mama akaja shuleni, polisi wakamkamata wakamchukua na kaka
wakawapeleka hospitali,” anasimulia Asha.
Anatoboa siri
Asha anasema mama yake alinunua panga na mkuki na kuuweka
ndani kwa lengo la kuwapigia.
Anasema tukio la kaka yake kuchomwa na mkuki lilikuwa la
kwanza. “Lakini mimi huwa akinifanyia hivyo mara kwa mara kwasababu hajanizaa
yeye, mimi ni mtoto wa kambo.
“Na wakati mwingine huwa ananipiga na ubapa wa panga.
Ametunza panga na mkuki ndani, huwa anatupiga kwa kutumia fimbo au ubapa wa
panga, alishawahi kunipiga hapa…(anaonyesha majeraha ya ubapa wa panga),”
anasema.
Anasema aliwahi kumtoboa na mkuki mkononi, pia mtoto huyo
anasema yeye ndiye mpishi hasa baba yake asipokuwapo.
“Nafanya kazi zote za nyumbani, kuosha vyombo, kupika,
kumlea mdogo wangu kufua nguo zetu na za mtoto,” anaelezea.
Said anasimlia
Anasema mama yake amekuwa mkatili na hana upendo kwa
watoto, kwasababu huwa anawapiga mara kwa mara tena kwa kutumia vitu vyenye
ncha kali.
Mama mzazi anena
Mariam anakiri kumchoma mkuki mtoto wake, lakini anadai
halikuwa kusudio lake bali ni bahati mbaya.
“Ni ajali tu sikuwa na wazo la kumchoma mwanangu,
nilitoka msibani nimechoka nikakuta hajafua nguo ndiyo nikachukua mkuki kumpiga
wakati najaribu kumchapa akajisogeza kwenye ncha ndiyo ukamchoma,” anasema.
Anasema hakujua kama mkuki huo umemjeruhi kiasi hicho,
hivyo alikwenda kulala na kuwaambia wapakue chakula wale.
“Nilishika mkuki akawa anataka kukimbia, nikamwambia
nitakuchapa akawa analia sikujua kama aliumia kiasi hiki,” anajitetea Mariam.
Mariam anakiri mtoto wake alipokwenda shule hakumwangalia
wala kumkagua, kwani alikuwa amelala ila alishangaa kuwaona walimu na polisi
wakija nyumbani kwake kumkamata.
Mwalimu anasemaje?
Mwalimu Catherine Matibijo aliyekuwa zamu, anasema
asubuhi wakiwa mstarini akikagua wanafunzi, alishangaa kumwona mtoto huyo
akitokwa na damu nyingi usoni.
“Nikamuuliza ilikuaje akaniambia alipigwa na mama yake
mzazi usiku, nikamruhusu aingie darasani kwanza,” anasema.
Alisema baadaye alienda kumwambia mwalimu wake wa darasa,
Theresia Makelele, walimchukua na kwenda naye kwa mwalimu mkuu.
“Tukaanza kumhoji, akasema ana dada yake wanasoma darasa
moja, tukamwita akatuelezea, tukampigia simu mama yao na kumwambia kuwa mtoto
anaumwa sana,” anasema Mwalimu Matibijo.
Anasema mama yake alitii na kufika, wakamuuliza na kukiri
kutenda kosa hilo kwa majibu ya dharau, wakamwacha arejee nyumbani na wao
wakaamua kutoa taarifa polisi.
Polisi, mganga wazungumza
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya Geita, Adam Sijaona
anakiri kumpokea mtoto huyo akiwa na majeraha eneo la usoni lililotokana na
kuchomwa na kitu chenye ncha kali. “Tulimpokea mtoto huyo na tumemshona nyuzi
sita, hali yake inaendelea vizuri,” anasema Dk Sijaona.
Ofisa wa Polisi Dawati la Jinsia, Butono Kasusula anasema
kosa alilolifanya Mariamu ni kinyume cha Sheria ya Mtoto kifungu Namba 21 ya
mwaka 2009.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment