Hoja za kisheria alizowasilisha Askofu wa
Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kuhusu kutakiwa kuwasilisha nyaraka
10 za utajiri na usajili wa kanisa lake polisi zimezaa matunda.
Sasa, agizo la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam la
kumtaka Askofu Gwajima kuwasilisha nyaraka hizo leo limesitishwa
kusubiri
utatuzi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali au Ofisi ya Mkurugenzi wa
Mashtaka.
Wakili John Mallya anayemtetea Askofu Gwajima alilieleza
gazeti hili jana usiku kuwa baada ya makubaliano na polisi mteja wake leo
hatafika Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kama ilivyokuwa
imepangwa mpaka hoja hizo za kisheria zitakapotolewa uamuzi.
Alhamisi iliyopita, polisi ilimtaka Gwajima kuwasilisha
vielelezo hivyo, lakini hatua hiyo ilipingwa na kiongozi huyo akieleza kuwa
hatapeleka nyaraka yoyote iwapo jeshi hilo halitajibu barua aliyoliandikia
kutaka liombe vitu hivyo kwa maandishi.
Nyaraka zilizotakiwa kuwasilishwa polisi ni hati ya
usajili wa kanisa, namba ya usajili, majina ya Baraza la Wadhamini (Baraza la
Kiroho), idadi ya makanisa (matawi) anayohudumia na nyaraka za helikopta ya
kanisa.
Nyaraka nyingine ni; muundo wa uongozi wa kanisa, waraka
wa maaskofu uliosomwa makanisa yote, nyaraka za nyumba na mali za kanisa,
nyaraka kuonyesha taarifa za hesabu kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Hiari na
kuambatana na mtu anayepiga picha za video kanisani hapo.
“Siwezi kuwasilisha kwa mdomo kwa kuwa hizi si mali za
Gwajima… ni mali ya taasisi na si vitu vyake binafsi,” alisema wakili huyo.
Katika barua yake kwa polisi, Wakili Mallya alisema:
“Tunaiomba Polisi kumwandikia rasmi mteja wetu kimaandishi nyaraka
mnazozihitaji na vifungu vya sheria vinavyotumika na polisi kutaka nyaraka
hizo… tutashukuru kupata hati hiyo.”
Kauli ya Kova
Mapema alipoulizwa kuhusu kitakachotokea leo, Kamanda
Kova alisema: “Suala la Mchungaji Gwajima kwenda na vielelezo alivyoagizwa na
Polisi siwezi kulizungumzia hadi hapo itakapotokea hakuja navyo ndipo
nitakapotoa tamko langu la mwisho.
“Nitazungumziaje hili? Si hadi itokee hakuja na vielelezo
na kama akija navyo halafu mimi nimeongea tofauti, nimeona italeta malumbano
kati yangu na yeye na mimi sitaki ifikie huko.
“Kuna mambo mengi ya kufanya hivyo nitalitolea tamko la
mwisho kwa waandishi wa habari kuhusu mchungaji Gwajima kama itatokea hivyo ili
tuendelee na mambo mengine.”
Kwa msisitizo zaidi
Mallya alisema nchi inaongozwa kwa sheria, hivyo kila
kitu kinatakiwa kiwe cha kisheria na kwamba wameiandikia polisi kuitaka waombe
nyaraka hizo kimaandishi na kuonyesha vifungu vya sheria vinavyowaongoza
kuziomba badala ya kusema kwa mdomo kwa sababu vitu hivyo ni vya kanisa na siyo
vya Gwajima peke yake.
Askofu Gwajima alihojiwa na Polisi, Kanda ya Dar es
Salaam kwa tuhuma za kumtolea maneno makali Polycarp Kardinali Pengo baada ya
kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki kutoa tamko lililotofautiana na la viongozi wa
Jukwaa la Wakristo Tanzania kuhusu suala la Katiba.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment