Mahakama Kuu Kanda ya Tabora imeiagiza Halmashauri ya
Wilaya ya Urambo, kuwalipa fidia ya Sh25 milioni Mwamini Adam na mumewe Idrisa
Jafari kutokana na madhara waliyopata baada ya uzembe uliofanywa na daktari wa
Hospitali ya wilaya hiyo alipokuwa akimfanyia upasuaji Mwamini.
Katika uamuzi wa shauri hilo la madai Namba 13/2011 uliotolewa juzi, Mahakama Kuu imeiagiza halmashauri hiyo kumlipa Sh20 milioni Mwamini aliyepata kilema cha maisha kwa kuondolewa mfuko wa uzazi na kukatwa utumbo.
Pia, mahakama imeiagiza halmashauri hiyo kumlipa fidia ya
Sh5 milioni Jafari ikiwa ni gharama za uendeshaji wa shauri hilo.
Akisoma hukumu, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya
Tabora, Amir Mruma alikubaliana na madai ya walalamikaji kuwa madhara
waliyopata kutokana na uzembe uliofanywa na Dk Jackob Kamanda ni makubwa.
Jaji Mruma alisema haipingiki kwamba huo ni uzembe
uliofanywa na mtumishi, hivyo mwajiri anapaswa kulipa gharama.
Aliagiza kuwa kiwango hicho cha fedha kitalipiwa riba ya
asilimia saba kila siku kuanzia tarehe ya uamuzi ulipotolewa hadi siku
mlalamikiwa atakapolipa fedha hizo.
Mwamini na mumewe walifikisha malalamiko yao Mahakamani
Kuu, wakidai kulipwa fidia ya Sh505 milioni kutokana na makosa ya uzembe
uliofanywa na wataalamu wakati wa upasuaji kwa kuacha kitambaa tumboni mwa
mgonjwa.
Wakili wa walalamikaji, Jaji Mussa Kwikima aliiambia
Mahakama kuwa uzembe huo umemsababishia kilema cha maisha mteja wake.
Awali, akiwaongoza wateja wake kutoa ushahidi, Wakili
Kwikima, waliieleza Mahakama kuwa baada ya kufanyiwa upasuaji, Mwamini
alihamishiwa Hospitali ya Rufani Kitete, lakini hali ilizidi kuwa mbaya
ikawalazimu kuhamia Hospitali ya Itigi kulikogundulika tatizo baada ya vipimo.
Walidai kuwa madaktari walibaini kuwa kulikuwa na kitu
ndani ya tumbo la Mwamini kilichokuwa kinasababisha atokwe na usaha sehemu za
siri na tumboni.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake, Anatory Lukonge
wa Hospitali ya Itigi ambaye alimfanyia upasuaji Mwamini katika ushahidi wake,
aliieleza mahakama kuwa walipomfanyia upasuaji walikuta utumbo umeshikana na
kizazi huku juu yake kukiwa na kitambaa.
Dk Lukonge alisema walikitoa kitambaa hicho lakini
kutokana na sehemu ya kizazi kuharibika, iliwalazimu kukiondoa huku akidai kuwa
hali hiyo ilisababishwa na uzembe wa daktari aliyemfanyia upasuaji.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment