Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), kimesema
kutosimamiwa vizuri kwa ratiba za mabasi za kuondoka eneo moja kwenda lingine,
ni miongoni mwa mambo yanayochangia ajali za barabarani kutokana na madereva
kukimbizana.
Kauli hiyo ya Taboa imekuja siku moja baada ya basi la
Nganga Express lililokuwa likitokea Kilombero kwenda Mbeya kugongana na lori
aina ya Fusso, kisha magari hayo kushika moto na kusababisha vifo vya watu 18.
Katibu Mkuu wa Taboa, Enea Mrutu alisema jana kuwa:
“Mfano hai yapo mabasi yanakwenda kwa kasi kutoka Dar es salaam hadi karibu na
Same mkoani Kilimanjaro ndiyo yanasimama porini ili kusubiri muda ufike,”
alisema.
“Ratiba ile inaonyesha kwamba ukitoka Ubungo saa fulani
unatakiwa kufika kituo B au C saa fulani. Sasa mabasi haya yanawahi tena wakati
mwingine saa mbili nzima...yanapita wapi? alihoji.
Alisema ajali nyingine zimekuwa zikisababishwa na makosa
ya kibinadamu ya madereva.
“Sisi tunasisitiza udereva uwe taaluma, tuachane na
madereva wanaopita magari mengine barabarani hata katika maeneo
yasiyoruhusiwa,” alisema Mrutu.
Hata hivyo, alitaja tatizo lingine kuwa ni miundombinu
mibovu ya barabara, akisema zina mashimo katikati na nyingine nyembamba.
Wakati huohuo, Chama cha Wasafirishaji Abiria (Akiboa),
mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara wamewatupia lawama askari wa usalama
barabarani.
Mwenyekiti wa Akiboa, Hussein Mrindoko aliwalaumu askari
hao kusahau kukagua malori na magari madogo ambayo nayo ni kiini cha ajali.
Mrindoko alisema mzigo mkubwa wanabebeshwa madereva wa mabasi tu.
Hata hivyo, Kaimu Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani,
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Johansen Kahatano alisema kuhusu
madai ya baadhi ya askari kutosimamia ratiba atachunguza.
Mmiliki wa mabasi ya Ngorika, George Temba alisema ratiba
ya mabasi zaidi ya 20 kuondoka muda mmoja ni tatizo.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment