Wanafunzi wa
vitivo vya Sayansi ya Afya wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Kampala-tawi la Dar es
Salaam (KIU), wamegoma kuendelea na masomo baada ya kubaini kuwa kozi
wanazosoma katika chuo hicho hazijasajiliwa katika ya bodi mbalimbali kama
taratibu na sheria zinazoelekeza.
Walianza mgomo huo tangu Ijumaa iliyopita baada ya
kugundua kuwa kozi wanazofundishwa hazijasajiliwa katika Bodi ya Mafamasia,
Bodi ya Maabara na Baraza na Madaktari.
Walisema jana chuoni hapo kuwa wamekuwa wakiendelea na
masomo bila kugundua kama kozi wanazochukua hazijasajiliwa katika bodi hiyo
huku uongozi wa chuo ukikaa kimya.
Waziri wa Afya wa Serikali ya Wanafunzi (KIUSO), Kenedy
Murunya, alisema walibaini kuwa kozi wanazosoma hazijasajiliwa baada ya kwenda
katika ofisi za bodi na kuelezwa kuwa hazijasajiliwa. Wanafunzi waliokumbwa na
tatizo hilo ni wale wanaochukua Shahada za maabara, udaktari na upasuaji.
“Wanafunzi walipokwenda Tume ya Vyuo Vikuu (TCU)
waliambiwa kuwa tume imeshafanya asilimia 50 ya usajili wa chuo hicho na asilimia
50 nyingine zilizobaki zinatakiwa zishughulikiwe na bodi husika za usajili,”
alisema.
Mwakilishi wa Kitivo cha udaktari (SUGA)), Martin
Augustine, alisema 2013 wakati wanaanza masomo waliambiwa na uongozi wa chuo
kuwa kozi zao zimesajiliwa bila kujua walikuwa wanadanganywa na
uongozi wa chuo hicho.
Alisema mwaka huu walikwenda Bodi ya Madaktari Tanganyika
wakaambiwa kuwa bado kozi yao haijasajaliwa kutokana na uongozi wa KIU kuzembea
kutuma nakala muhimu zitakazofanikisha usajili.
Alisema Ijumaa baada ya mgomo wawakilishi wa vitivo vya
sayansi wa ngazi zote za masomo walifanya kikao na uongozi wa chuo chini ya OCD
wa Ilala kujadili matatizo ya usajili na uongozi na kuwa cha ajabu wawakilishi
hao hawakupewa majibu yanayoridhisha hali iliyosababisha mgomo huo kuendelea.
Alisema tangu mgomo uanze Jeshi la Polisi limeweka kambi
likiangalia hali ya usalama wa chuo.
Alisema Septemba, 2014 walikwenda Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi kwa lengo la kumuona Waziri, Dk. Shukuru Kawambwa, lakini
hawakumuona hivyo kumwandikia barua ili
awape majibu ambayo hadi sasa hawajapatiwa.
Alisema wanaendelea kulipa ada kubwa japokuwa serikali
ilikiagiza chuo hicho kushusha ada cha kushangaza Baraza la KIU ambalo lipo
Uganda lilikataa maagizo ya serikali.
Alisema wanafunzi wa udaktari mwaka wa pili wanalipa Sh.
milioni 8 wakati wa mwaka kwanza wanatozwa Sh. milioni 6.7, maabara sh. milioni
4.8, Famasia milioni 5.4 huku wa mwaka wakilipa sh. milioni 3.8.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu wa KIUSO, Elisha Mushi, mgomo
huo unajumuisha wanafunzi wa vitivo vya sayansi pekee wakati vitivo vya
biashara na sharia vinaendelea na masomo.
Hadi tunakwenda mitamboni, jitihada za kumpata Rais wa KIUSO, Elias Mbogo pamoja na
Waziri wa Elimu, Answari hazikufanikiwa baada ya kuambiwa kuwa wote wamekwenda
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupata ufumbuzi wa matatizo ya wanafunzi.
Hata hivyo, Naibu Waziri wa Elimu wa Kiuso, Fadhilina
Kassim, alisema anachofahamu yeye kuwa chuoni hapo kuna mgomo wa wanafunzi,
lakini mwenye dhamana ya kuzungumzia suala hilo ni Waziri wa Elimu au Waziri
Mkuu.
Afisa Masoko na Uhusiano wa KIU, Keneth Uki, alithibitisha
kuwapo kwa mgomo wa wanafunzi hao huku akisisitiza kuwa vitivo vingine vya
sayansi vimeshakamilika usajili ingawa kitivo cha wanafunzi wanaochukua Famasia
tu ndio kozi zao hazijakamilisha usajili katika Baraza la Famasia Tanzania.
Wanafunzi hao wanaiomba wizara husika iwapatie ufafanuzi
kuhusiana na suala hilo pamoja na uhalali wao KIU kwa kuwa walijiunga na chuo
hicho kupitia TCU na NACTE.
NIPASHE
No comments:
Post a Comment