Asasi zisizo za kiserikali 53 zimemwandikia Rais Jakaya
Kikwete, barua ya kumuomba asisaini Sheria ya Takwimu ya 2015 na Sheria ya
Makosa ya Mtandaoni zilizopitishwa na Bunge hivi karibuni ili kuruhusu
kufanyiwa marekebisho kwanza.
“Tunashauri kabla ya kutia saini sheria hizi upate muda
wa kusikiliza kilio cha jamii juu ya ubaya wa sheria hizi kwa mustakabali wa
taifa. Sheria hizi zikipitishwa katika utawala wako zitatia doa dhamira yako
nzuri ya kuongeza wigo na uhuru wa habari na ushiriki wa wadau katika maendeleo
ya kitaifa,” alisema.
Barua hiyo imeeleza sababu za kumtaka Rais kutosaini
sheria hizo kuwa ni, malengo ya Sheria ya Takwimu siyo tu kuratibu takwimu za
kitaifa, bali umetoa madaraka makubwa kwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kama
kitovu cha utoaji wa takwimu nchini.
“Maana yake ni kwamba taasisi zote za serikali, mashirika
binafsi, taasisi za elimu ya juu, vyuo vikuu na taasisi za utafiti hazitakuwa
na uhuru wa kutoa matokeo ya tafiti wanazozifanya bila ya kibali au ridhaa ya
NBS” ilisema barua hiyo.
Imesema pia sheria hiyo imeweka adhabu kali kwa vyombo
vya habari, asasi za kiraia, taasisi za utafiti na vyuo vya elimu ya juu
vitakavyotenda makosa yaliyoainishwa katika sehemu ya tatu ya sheria.
Kuhusu Sheria ya Makosa ya Mitandao, barua hiyo imesema
itaminya kwa kiasi kikubwa uhuru wa wananchi kuwasiliana na kupashana habari
endapo itasainiwa bila marekebisho.
“Ni dhahiri sheria hii imelenga kufuta kabisa uhuru wa
mawasiliano na matumizi ya mitandao ya kijamii kama Facebook, WhatsApp, Jamii
Forums, Twitter, blog… Kupitishwa kwa sheria hii bila kufanyiwa marekebisho
kutasababisha Watanzania wengi kutiwa hatiani bila sababu, lakini pia kutaondoa
kabisa uhuru wa habari nchini” iliongeza kusema.
No comments:
Post a Comment