ASKOFU wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima
amezua jambo baada ya kuhusishwa na kauli ya Serikali kuhusu kuzifungia taasisi
mbalimbali zikiwamo za kidini.
Hatua ya Askofu Gwajima kuziponza taasisi hizo,
imetafsiriwa na viongozi wa dini siku moja baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi, Mathias Chikawe kutangaza tishio la kuzifuta taasisi hizo.
Kutokana na hatua hiyo, viongozi wa dini wamemtaka Waziri
Chikawe kufuta kauli yake ambayo wamesema ina vimelea vya mgogoro uliopo baina
ya Serikali, Askofu Gwajima na tamko lililotolewa na Jukwaa la Wakristo
Tanzania (TCF) kuwataka wananchi kuipigia kura ya hapana Katiba
Inayopendekezwa.
Juzi, Waziri Chikawe alisema sababu kubwa ya kutaka
kuzifuta taasisi hizo ni kujihusisha na kazi nyingine kinyume cha sheria za
vyama vya kijamii sura ya 337 na kanuni zake zinazosimamia uendeshaji wa
taasisi hizo.
Askofu Mwamalanga
Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, Amani na Haki za
Binadamu kwa Jamii ya Madhehebu ya Dini, Mchungaji William Mwamalanga,
aliliambia MTANZANIA kuwa kauli ya Serikali imejaa vitisho kwa raia wake na
inaonekana wazi inataka kuwatenganisha na Serikali yao.
Alisema tamko hilo limekuja baada ya mlolongo kati ya
Serikali na Askofu Gwajima ambapo alimshauri waziri kuziita taasisi zote kabla
ya uamuzi wa kuzifuta.
“Nafikiri jambo hili lina uhusiano na mgogoro kati ya
wizara na Askofu Gwajima, cha kustaajabisha kama kulikuwa na tofauti hizo kabla
kwa nini walimhifadhi hadi sasa.
“Wangetatua mambo yao kuliko kutumia kivuli cha Askofu wa
Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhana Kardinali Polycarp Pengo
kudhalilishwa… hapa Serikali inataka kuigawa jamii,” alisema Mchungaji
Mwamalanga.
Alisema kauli ya Waziri Chikawe ina nia ya kuiondoa
Serikali mioyoni mwa wananchi wake.
Mchungaji Mwamalanga alisema wakati huu ambao nchi
inaelekea uchaguzi mkuu, wasingependa kuona makundi ya hasira yanazaliwa.
Alisema matamko yoyote yanapaswa kuwa ya kujenga na si
kila kukicha kuzalisha mitafaruku.
Askofu Mgulu
Mchungaji wa Kanisa la Christian Ministry Fellowship,
Askofu Dk. Mgulu Killimba, naye alisema inawezekana chanzo cha kauli hiyo ni
Askofu Gwajima na tamko la TCF hatua inayosababisha Serikali kutaka kushusha
rungu.
Alisema taasisi za dini zipo kuikosoa Serikali kwa nia ya
kujenga, ingawa Serikali sasa inataka kuwanyamazisha Watanzania jambo ambalo si
zuri.
“Jukwaa limeleta msimamo wake kuhusu Katiba
Inayopendekezwa, wanasema wengi wape, kama jukwaa tulitoa msimamo wetu huenda
tumeenda kinyume na matarajio yao, mtu anayekupinga asitazamwe kama adui,
tusitumie njia hizo kuwagawa Watanzania ambao wameelimika kwa sasa.
“Taasisi za dini zipo kwa mujibu wa sheria, unapozifungia
maana yake zisifanye kazi kwa uhuru, labda waunde sheria mpya.
“Kuna mambo mengi ya Serikali kushughulikia, lakini
inalegalega kwa mfano tatizo la rushwa liko kila mahali unapokwenda, ebu waanze
na hili kwanza,” alisema.
Kuhusu kupeleka ‘return’, alisema hawana ruzuku kama
vyama vya siasa, lakini kama wanataka kukaguliwa wanawakaribisha.
Askofu Niwemugizi
Naye Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Rulenge mkoani
Kagera, Severine Niwemugizi, alisema tamko la kuzifungia taasisi za dini
zitakazotoa maelekezo kwa waumini wao juu Katiba Inayopendekezwa ni kwenda
kinyume na sheria ya kura ya maoni.
Askofu Niwemugizi ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Baraza
la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), alisema sheria ya kura ya maoni
inaeleza wazi kuwa kutakuwa na makundi mawili yatakayoipigia kampeni Katiba
Inayopendekezwa.
Alisema kwa hali hiyo, Serikali itarajie upinzani mkubwa
kutoka kwenye taasisi hizo kwani wanajua kuwa sheria inawaruhusu.
Hata hivyo, alisema anashukuru Serikali kutoa kauli hiyo
kwani itasaidia wao kuanza kujipanga vizuri.
Jukwaa la Katiba
Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Hebron
Mwakagenda, alisema tamko hilo ni vitisho baada ya kuona joto la mwamko wa
wananchi limepanda.
Alisema Serikali inajaribu kutisha wananchi ili
wakubaliane na kila jambo ambalo wanalitaka viongozi wa juu.
“Tukiangalia kwa kina jambo la Katiba, wananchi wanapaswa
kuelewa kuwa kura ya ndiyo haimilikiwi na Serikali, bali kura ya ndiyo au
hapana ni uamuzi wa wananchi wenyewe,” alisema.
Kuhusu taasisi za dini kujihusisha na siasa, alisema
inapaswa Serikali na wananchi waelewe ni siasa ya aina gani inayozungumziwa,
kwani masuala ya Katiba ni ya wananchi wote, si ya vyama vya siasa tu.
Kituo cha Sheria
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu (LHRC), Dk. Helen Kijo-Bisimba, alisema ameshangazwa na Waziri Chikawe
ambaye kitaaluma ni mwanasheria kutangaza hatua hiyo.
“Sioni mantiki kubwa ya kutaka kuzifungia taasisi hizi,
zaidi ya kutaka kukomoana na kutishia ili taasisi zinazoeleza ukweli wa mambo
zikae kimya,” alisema Dk. Kijo-Bisimba.
MTANZANIA
No comments:
Post a Comment