Siku tano baada ya Rais Jakaya Kikwete kusema kuwa tamko
la Jukwaa la Wakristo (TCF) kuwataka waumini wao kupigia kura ya ‘hapana’
Katiba Inayopendekezwa lilikuwa la hasira, viongozi hao wamejitokeza tena na
kusisitiza kwamba msimamo wao huo utabaki kama ulivyo.
Katika tamko pamoja walilolitoa jana baada ya kukutana
juzi mjini Dodoma, viongozi hao wamemtahadharisha Rais Kikwete kuwa kuendelea
kupigia debe Katiba Inayopendekezwa na kuruhusu Mahakama ya Kadhi, kunaweza
kulitumbukiza Taifa katika machafuko na hali ikiwa hivyo Serikali ndiyo
itakayolaumiwa.
Tamko hilo limesainiwa na viongozi walewale waliosaini
lile la awali la Machi 12, mwaka huu ambao ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo
Tanzania (CCT), Askofu Dk Alex Malasusa, Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa
Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa na Mwenyekiti wa
Kanisa la Pentekoste Tanzania (CPCT), Askofu Daniel Awet.
Tamko hilo la maneno 921, limeendelea kuwataka waumini
wao kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura,
kuisoma Katiba Inayopendekezwa na kujitokeza kuikataa kwa kupiga kura ya
‘hapana,’ msimamo ambao tayari umeibua msuguano baina yao na Askofu Mkuu wa
Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo
aliyesema viongozi wa dini hawana mamlaka ya kuwaamulia waumini wao aina ya
kura wanayostahili kupiga.
Pia, Jukwaa hilo limewataka viongozi wakuu wa Serikali
–Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Rais Kikwete wasifurahi kwamba ujumbe wao
umewafikia viongozi wa dini waliozungumza nao hivi karibuni, kwa kuwa watu
waliokutana nao si wawakilishi rasmi na hawana uwezo wa kutoa uamuzi au
kukubaliana juu ya jambo la kitaifa.
“Maaskofu tuliokutana hapa (mjini Dodoma) hatuna hasira
na wala hatuongozwi na hasira wala mihemko katika kufikia maamuzi tunayofanya
kama ambavyo wengine wanavyotutafsiri, tunafikia maamuzi yetu baada ya maombi
na sala na tunasukumwa na upendo kwa wananchi ili kujenga Taifa lenye umoja,
amani, utulivu na maelewano,” lilisema tamko hilo likihitimishwa kwa maneno ya
Biblia kutoka Mithali 29: 1, “Aonywaye mara nyingi akishupaza shingo,
atavunjika ghafla, wala hapati dawa.”
Jumamosi iliyopita, Rais Kikwete akifungua mkutano wa
Kamati ya Amani ya Mkoa wa Dar es Salaam iliyoshirikisha wajumbe kutoka mikoa
mbalimbali ikijumuisha viongozi wa dini za Kiislamu na Kikristo, alisema
msimamo wa TCF kuhusu kuipigia kura ya ‘hapana’ Katiba Inayopendekezwa ni wa
hasira na usiokuwa na tija kwa maendeleo ya Taifa.
“Nimeyasoma matamko hayo yote kwa umakini, imenishangaza,
imenisikitisha na kunihuzunisha. Siamini kwa nini wamefikia huko kwa kuunga au
kutokuunga mkono,” alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete alisema: “Waacheni waumini waamue Katiba
wanayoitaka wao... hayo matamko niliyoyasoma yamejaa hasira kwa Serikali
kupeleka bungeni Muswada wa Mahakama ya Kadhi.”
Maaskofu hao walikuwa Dodoma kufuatilia kwa kina Muswada
wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali ya mwaka 2014 unaopendekeza, pamoja na
mambo mengine, marekebisho ya Sheria ya Tamko la Sheria za Kiislamu la mwaka
1964 unaotambua Mahakama ya Kadhi.
“Muswada huu unapendekeza kuanzishwa Mahakama ya Kadhi
ambao utawasilishwa bungeni leo kwa hati ya dharura na hivyo kuufanya umma wa
Watanzania kutokujua maudhui yaliyomo katika muswada huo wakati bado hoja zetu
za msingi tulizopeleka kwenye Kamati ya Katiba na Sheria ya Bunge na kwa Waziri
Mkuu hazijajibiwa,” Ilieleza taarifa hiyo.
“Tunamtaka Rais aagize muswada huu uondolewe bungeni na
usijadiliwe tena kwa kuwa utafiti wa Tume ya kurekebisha sheria ulishaonyesha
madhara ya uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi. Vinginevyo, kuendelea kujadiliwa
kwa muswada huu maana yake ni kwamba Serikali inajihusisha na itagharimia
mahakama hiyo.”
Walisema; “Yalijitokeza kwenye semina kwa wabunge
mwishoni mwa wiki ni ishara ndogo ya kile kitakachotokea maeneo yote ya nchi
yetu. Hapa tunajiuliza, endapo maneno ya Rais ni kweli, mbona Bunge linaendelea
kujadili kitu ambacho Serikali haitajihusisha wala kukigharamia?”
Tamko hilo lilionya: “Tunamtaka Rais (Kikwete) aiepushe
nchi yetu na kuingizwa kwenye mapigano ya kidini ambayo kuyadhibiti itakuwa
vigumu. Pia tunamwomba Rais Kikwete akumbuke na kutafakari kile kilichotokea na
kinachotokea nchi ya Afrika ya Kati, kati ya kundi la Seleka na kundi la Anti
Balaka.
Bunge laondoa Muswada wa Mahakama ya Kadhi
Hata hivyo, taarifa zilizopatikana bungeni jana na
kuthibitishwa kwa nyakati tofauti na Naibu Spika, Job Ndugai na Katibu wa
Bunge, Dk Thomas Kashillilah zilisema kuwa muswada huo hautajadiliwa katika
mkutano wa 19 wa Bunge unaomalizika leo, badala yake utapangiwa siku nyingine.
“Suala la Mahakama ya Kadhi halitawasilishwa bungeni tena
mpaka hapo litakapopangiwa siku nyingine. Hata Waziri Mkuu (Mizengo) Pinda
wakati akizungumza katika semina ya wabunge aliliweka sawa suala hili. Kwa
kauli alizozitoa hakuna haja tena ya kuhoji kama suala hili litakwenda bungeni
au la,” alisema Kashillilah.
Ndugai alisema ni vigumu kwa suala hilo kuwasilishwa
bungeni na kwamba litajadiliwa katika vikao vijavyo vya Bunge.
Mikutano ya viongozi
Maaskofu katika tamko lao, walisema wameshangazwa na
tabia ya viongozi wa Serikali ya kuitisha na kuendesha mikutano wanayodai ni ya
viongozi wa dini lakini isiyo rasmi.
“Machi 03, 2015 Waziri Mkuu (Pinda) aliitisha mkutano
kupitia mchungaji mmoja ambapo hakuna hata kiongozi mmoja wa taasisi au kanisa
aliyeshiriki. Jambo la kushangaza ni kile kilichotokea Machi 28, 2015 ambapo
Rais Kikwete alishiriki kikao cha kikundi ambacho siyo rasmi, yaani Kamati ya
Amani ya Mkoa wa Dar es Salaam.
“Mikutano ya jinsi hii kati ya Serikali na wale ambao
imewaona kuwa ndiyo viongozi wa dini siyo sahihi kwani viongozi wa dini wana
taratibu zao za kualikwa au kuwakilishwa katika mikutano na viongozi wa
Serikali au wa dini au madhehebu mengine.
“Kwa mantiki hiyo tunawashauri viongozi wa Serikali
waache kabisa kutumia vikundi visivyo rasmi kualika mikutano wanayodhani kuwa
itakubalika na waumini wa dini hizo. Mikutano yote ya jinsi hiyo itakayoitishwa
ni batili na maamuzi yake hatuyatambui na hatutayatambua.”
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment