MTOTO wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, Jaji Joseph Warioba amejiunga na Chama cha Alliance for Change
&Transparency-Tanzania (ACT).
Binti huyo aliyejiandikisha kwa jina la June Warioba,
alichukua kadi ya kujiunga na chama hicho makao
makuu ya chama hicho
Kijitonyama mjini Dar es Salaam jana.
Hata hivyo, June alikataa kupigwa picha wala kuzungumza
na waandishi wa habari waliokuwapo ofisini hapo.
Aliingia ofisini hapo saa 4 asubuhi ambapo alitumia
takribani nusu saa kufanikisha usajili wa chama hicho na kutoka ndani akiwa
ameongozana na Katibu Mwenezi wa chama hicho, Msafiri Mtemelwa.
June alikuwa amejiziba uso kwa mkono ili asipigwe picha
wala kuulizwa maswali ambapo aliingia kwenye gari na kuondoka.
Alipoulizwa kwanini amejiunga na chama hicho kimya kimya
na kwa haraka, alisema huo ni uamuzi wake.
Naye Mwenyekiti wa ACT, Anna Mughwira alisema
June
hakutaka kuandikwa kwenye vyombo vya habari,hivyo waliheshimu uamuzi wake huo.
Alisema kila mwanachama ana uhuru wa kuamua namna ya
kujiunga, kwani wapo wanataka waandikwe au kutangazwa na vyombo vya habari na
wengine hawapendi.
“Si mtoto wa Warioba, ni mwanachama wa kawaida tu
hajasema chama alichotoka wala hajaweka wazi kama anataka kugombea nafasi
yoyote ya uongozi na hakupenda kuandikwa ni kama mimi nilivyoingia.
“Sisi tuna wanachama mbalimbali, siku ya uzinduzi kuna
wengine walikuja na kadi zao wakitaka kujiunga,hatutaki ugomvi na vyama pinzani
vingine kwa sababu sisi pia ni wapinzani,” alisema.
Jaji Warioba anena
Akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya simu, Jaji Warioba
alikiri June ni mtoto wake wa kumzaa.
Kuhusu uamuzi wake wa kujiunga na ACT, Jaji Warioba
alisema aachiwe mwenyewe.
“Yule ni mtu mzima, hayuko chini yangu na ana uamuzi
wake… siwezi kumwingilia uhuru wake,” alisema Jaji Warioba.
No comments:
Post a Comment