Tukio la kijana mwanafunzi Mtanzania, Rashid Charles
Mberesero kukamatwa nchini Kenya akihusishwa na shambulizi la kigaidi katika
Chuo Kikuu cha Garissa kilicho kaskazini mwa nchi hiyo jirani, haliwezi kupita
kirahisi bila watu binafsi, taasisi za serikali na umma kwa ujumla kufanya
tathmini ya kina.
Tathmini ya kina ya kujiuliza, ni vipi kijana mdogo kama
huyo, ambaye alikuwa mwanafunzi wa kidato cha tano katika Shule ya Sekondari
Bihawana ya mkoani Dodoma, kushiriki katika jambo kubwa na baya tena la kinyama
kama hilo, bila watu wake wa karibu, taasisi za usalama na hata majirani
kutilia shaka nyendo zake.
Kwa mujibu wa mama yake mzazi, kijana huyo mwenye umri wa
miaka 20, kutoka Same mkoani Kilimanjaro, hakuwahi hata kufika jijini Dar es
Salaam, sembuse kuvuka mpaka na kuingia nchi nyingine. Nyendo zake, ni kutoka
huko kwao kuelekea shuleni Dodoma.
Kama utamwelewa vizuri mama huyo pamoja na simulizi ya
walimu kutoka shuleni kwao na wanafunzi wenzake, ni kwamba endapo Rashid
alipata mafunzo yoyote ya kutumia silaha na ugaidi, basi mambo haya yamefanyika
ndani ya ardhi ya Tanzania, tena katika mikoa kati ya Kilimanjaro na Dodoma!
Tunaweza kuliona jambo hili kuwa ni dogo na la kawaida
labda kwa kuwa kijana huyu amekwenda kutekeleza vitendo vyake viovu nje ya nchi
yetu, lakini kwa watu makini tunaotazama kwa macho matatu, suala hili siyo dogo
kabisa, ni kubwa linalopaswa kuwaumiza vichwa watendaji wa taasisi zetu za
ulinzi na usalama, sambamba na wananchi wenyewe kwa ujumla wao.
Kumbe, katika sebule zetu, ndani ya nyumba zetu na hata
mapori yetu, bado kuna watu wanaweza kuwafundisha vijana wetu wa sekondari na
vyuo, kuasi taifa lao, kusaliti ubinadamu wao na kujiingiza katika mambo maovu
kama anavyotuonyesha Rashid!
Wananchi, labda kwa kutingwa na harakati za kujitafutia
mlo wao wa kila siku, wameacha kuwa na macho ya udadisi, hawashangai tena
wanapoona jambo lisilo la kawaida linapoendelea.
Ingekuwa zamani, watu wangetilia shaka nyendo za Rashid
kupenda kushinda msikitini na kuwa mtu wa peke yake, peke yake!Hata vyombo
vyetu vya usalama, navyo vinaonekana vimelala, havijishughulishi tena na mambo
magumu, badala yake wamekuwa na intelijensia kali kufuatilia wanasiasa, hasa wa
upinzani ambao shughuli zao nyingi ni za wazi.
Wanausalama wetu ni wepesi kufahamu vurugu zitakazotokea
katika maandamano ya walimu wanaodai malimbikizo ya mishahara yao, kuliko kuhisi
juu ya kuwepo kwa watu wanaotoa ufadhili wa walimu wa maovu kwa vijana wetu.
Kama vijana wetu wa sekondari wanaweza kuingiliwa na
kushawishiwa hadi kukubali kufanya ugaidi, sioni wahalifu hawa kama watapata
kazi kubwa kuwashawishi kushika silaha mamia ya vijana wasio na kazi
wanaoshinda vijiweni na kukaba watu usiku kwa ahadi tamu zisizo na ukweli
wowote.
Tuna-relax labda kwa vile wanaoshambuliwa hivi sasa ni
Wakenya. Tunasahau kuwa wapo Wakenya ndani ya kundi la Al Shabaab.Kwa tukio la
Rashid nashawishika kuamini kwamba ndani ya kundi la Al Shabaab kuna Watanzania
sasa ni juu ya serikali na vyombo vyake vya usalama kufuatilia kiintelejensia
ili kubaini hili haraka sana kabla mambo hayajaharibika.
Inashangaza, Rashid alikuwa akisoma katikati ya nchi yetu,
Dodoma, ilikuwaje hao Al Shaabab wakaingia Bihawana na kumshawishi kijana huyo
bila kugundulika? Ilikuwaje Rashid akasafiri hadi mashariki mwaka Kenya
akitokea Tanzania bila kujulikana na vyombo vyovyote vya dola?
Hii maana yake ni kwamba kuna watu wanaosuka mipango na
kufanikisha vijana kuvuka mipaka na kwenda kujiunga na Al Shaabab, sasa ni nani
hao? Watafutwe kwa sababu wanahatarisha usalama wa taifa letu.
Hao ndiyo wanaosababisha vijana wetu kuingia katika
mzunguko wa magaidi na siku watakapoanza kutushambulia, wapo baadhi ya vijana
wetu, wanaopata mafunzo humu humu nchini, watatumika kutuua na tutakuwa
tumechelewa kuwadhibiti! Nashauri hili nalo lionekane kama ni janga la taifa na
lipigwe vita.
GPL
No comments:
Post a Comment