Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Ernest Mangu akitoa
hotuba yake katika Mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi wa dini ya Kiislam
katika kuimarisha usalama nchini yakiwa na kauli mbiu isemayo “Amani na usalama
ndio maisha yetu”.
Na Frank Geofray- Jeshi la Polisi.
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Ernest Mangu pamoja na
viongozi wa dini ya Kiislamu nchini wameungana kwa pamoja kukemea vitendo vya
uhalifu hapa chini pamoja na kuzitaka familia kutoa malezi bora kwa watoto wao
ili kuondokana na wimbi la watu wanaojiingiza katika vitendo hivyo.
Rai hiyo ilitolewa leo jijini Dar es salaam na IGP Ernest
Mangu pamoja na Viongozi mbalimbali wa dini ya kiislamu katika muendelezo wa
Mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi wa dini hiyo katika kuimarisha usalama
nchini yakiwa na kauli mbiu isemayo “Amani na usalama ndio maisha yetu”.Mafunzo
ambayo yaliratibiwa na Taasisi ya Mwinyi Baraka na kuhudhuriwa na viongozi
mbalimbali wa dini ya kiislamu hapa nchini.
IGP Mangu alisema Viongozi wa dini wanadhamana kubwa
katika kuhakikisha kuwa vitendo vya uhalifu vinadhibitiwa nchini kwa
kuwaelimisha waumini wao na jamii kwa ujumla juu ya madhara ya uhalifu pamoja
na kuwapa mafundisho yatakayojenga na kuimarisha ulinzi na usalama nchini.
Alisema wahalifu wa sasa wana mbinu nyingi hivyo kitu kikubwa
kitakachoweza kusaidia katika mapambano hayo ni mshikamano wa dhati kutoka kwa
viongozi hao katika kuwafichua ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Naye Mwakilishi wa Sheikh Mkuu wa Tanzania katika kikao
hicho ambaye ni Mjumbe wa Baraza kuu la ulamaa BAKWATA, Sheikh Abubakar Zuber
alisema kuna haja ya kuziba nyufa za uvunjifu wa amani ambazo zimeanza
kujitokeza hapa nchini.
Alisema ni muhimu kuziba nyufa hizo kwa kuanzia kwenye
misikiti, familia zao na hatimaye katika jamii zinazowazunguka ili kuhakikisha
kuwa nchi inaendelea kubaki salama kwakuwa amani tuliyo nayo ni neema ambayo
tunapaswa kuilinda kwa nguvu kubwa.
“Vilevile hatuna budi kuimarisha malezi katika familia
zetu mana tunaposhindwa kuwalea watoto wetu vizuri ndio chimbuko la kushamiri kwa
vitendo vya uhalifu wa aina mbalimbali hivyo tujielekeze katika kutoa mafunzo
bora katika familia”Alisema Sheikh Zuber.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wanazuoni wa
Kiislamu Sheikh Khamis Mataka alisema uhalifu unaweza kujitokeza sehemu yeyote
na hata ndani ya msikiti hivyo ni jukumu la viongozi wa misikiti kuwafichua
wahalifu walio ndani ya misikiti.
Akizungumzia mafunzo hayo Mwenyekiti wa Taasisi ya
Mwinyibaraka Sheikh Issa Othman alisema wataendelea kutoa mafunzo hayo ili
kuwajengea uwezo viongozi wa dini waweze kuwaelimisha waumini wao juu ya
kukabiliana na vitendo vya uhalifu ili kuimarisha ulinzi na usalama.
MICHUZI
No comments:
Post a Comment