MWALIMU wa Madrasa, Alhaji Maulana Shiraz (71) wa Jumuiya
za Wi’yatu LiQadria iliyoko kijiji cha Chikundi wilayani Masasi mkoa wa Mtwara,
anashikiliwa na Jeshi la Polisi wilaya ya Masasi kwa tuhuma za kukutwa na
watoto wadogo wapatao 11, wa kike na wa kiume, kinyume na taratibu na sheria za
nchi.
Pia, amekutwa na fomu za usajili zinazoonesha
taarifa muhimu za mwanafunzi hao, zikiwemo jina la mtoto, jina la mzazi, mahali
anakotoka kwa maana ya kijiji na kata pamoja na mawasiliano ya mzazi au mlezi
wa mwanafunzi.
Watoto waliokutwa katika kituo hicho ambao
wanatoka katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya Lindi na Mtwara ni Selemani Juma
(12) wa kijiji cha Mandawa, Ruangwa, Bakari Nang’ani (12) anayetoka pia
Ruangwa, Jamal Abbas (12) na Mwajuma Selemani (12) wanaotoka Mwena, Masasi,
Karim Abbas (17) mkazi wa Liwale mkoani Lindi.
Wengine ni Mark Muhidin (12), Haji Juma (18),
Ganafi Hamisi (13) na Murji Muhidin (12), wakazi wa kijiji cha Mkululu wilayani
Masasi, Nurdin Ausi (11) kutoka kijiji cha Mpanyani, Masasi na Ally Bakari (12)
mkazi wa kijiji cha Milola mkoani Lindi.
Pia yumo Hamis Seif (05) mkazi wa kijiji cha
Kanyimbi wilayani Masasi katika mkoa wa Mtwara.
Jeshi la Polisi wilayani Masasi limethibitisha
tukio hilo kupitia kwa Kaimu Mkuu wa jeshi hilo wilaya ya Masasi, Nathanael
Kyando na kusema linamshikilia mtuhumiwa huyo kwa mahojiano zaidi ili kubaini
alikuwa na nia gani juu ya watoto hao.
Akizungumza na HABARI LEO, Alhaji Maulana
alikiri kukaa na watoto hao walioletwa na wazazi na walezi wao kwa zaidi ya
miezi miwili nyumbani hapo kwa madai ya kuwapa elimu ya dini ya Kiislamu kwa
muda wa miaka mitatu ili aweze kupata thawabu kutoka kwa Mungu.
Alisema hakuwa na nia mbaya ya kukaa na watoto
hao, ingawa amekiri kufanya makosa ya kukaa na watoto ambao walistahili kuwepo
shuleni kupata elimu dunia.
Aliomba Jeshi la Polisi limwachie huru, kwa kuwa
alichokitenda ni moja ya ahadi ambayo aliiahidi kuwa ataitimiza mara tu baada
ya kurejea kutoka kwenye “Ibada ya Hijja” mwaka 2013.
Alhaj Maulana alisema alianza kukaa na watoto
hao Desemba mwaka jana kwa makubaliano na wazazi wao kuwa masomo chuoni hapo,
yataanza rasmi Januari 30, 2015 huku moja ya sharti la chuo likiwa ni mzazi
kugharimia matibabu ya mtoto wake pindi atakapolazwa.
Katika hali ya kushangaza ni pale Katibu Tawala
wa Wilaya ya Masasi, Danford Peter alipoamua kupiga moja ya namba ya simu ya
mzazi wa mtoto, Ally Bakari (0783-812523) anayetoka kijiji cha Milola, Lindi
aliyefahamika kwa jina la Bakari Mtapila.
Mtu huyo alipopokea simu, alikana kuwa jina hilo
si lake na hana mtoto mwenye jina hilo anayeishi Masasi, licha ya kukiri kuwa
ni mkazi wa Milola.
Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Bernard Nduta,
aliyekuwepo eneo la tukio, alisema wao kama serikali wameviagiza vyombo vya
dola kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tuhuma hizo na hatimaye watatoa taarifa
rasmi kwa vyombo vya habari.
Ofisa Ustawi wa Jamii kutoka Halmashauri ya
Wilaya ya Masasi, Thabit Thabit alisema mzee huyo ametenda kosa la kukaa na
watoto hao, ambao amewakosesha haki zao za msingi ikiwemo elimu.
No comments:
Post a Comment