UKWASI wa Kiongozi Mkuu wa Chama Cha Alliance for Change
and Transparency(ACT Wazalendo), Zitto Kabwe umeongezeka kutoka umiliki wa
shamba moja na Sh milioni 30 alizokuwa amezihifadhi katika akaunti za benki
mbili tofauti hapa nchini, na sasa anamiliki mali na fedha zinazofikia Sh
milioni 690, MTANZANIA Jumamosi linaripoti.
Kwa mujibu wa taarifa hizo mpya alizoziweka hadharani
wiki hii katika fomu maalum ya kuonyesha mali zinazomilikiwa na viongozi wa chama
hicho, Zitto ametanabaisha kuwa kwa sasa anamiliki nyumba mbili.
Nyumba hizo, moja ina thamani ya Sh milioni 180 na
nyingine Sh milioni 43, Pia anamiliki kitalu cha ekari 12 ambacho kinathamani
ya Sh milioni 25, vyote vikiwa Mwandiga mkoani Kigoma.
Zitto pia ameweka hadharani kumiliki mashamba matatu
katika mikoa ya Kigoma, Mtwara na Dar es Salaam.
Katika ufafanuzi wake kuhusu mashamba hayo, Zitto
ameeleza kuwa anamiliki shamba la ekari sita katika manispaa ya mji wa Mtwara
likiwa na thamani ya Sh milioni 60.
Hali kadhalika shamba lingine la ekari tatu lenye thamani
ya Sh milioni 20 huko Matyazo Kigoma, lingine la ekari 3 lenye thamani ya
shilingi milioni 90 ambalo liko Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Katika fomu hiyo, Zitto alijaza kuwa anamiliki pia gari
moja aina ya Land Lover, Free Lander ambalo alinunua kwa dola za Kimarekani
40,000 sawa na Sh. milioni 72.
Kwa upande wa fedha alizokuwa nazo wakati anajaza fomu
hiyo ni Sh. milioni 18, pia alitanabaisha kuwa amehifadhi fedha katika Benki ya
CRDB, NMB na STANBIC zenye jumla ya Sh milioni 9.8.
Zitto pia aliweka wazi kumilika shirika lisilo la
kibiashara la Kigoma Development Initiatives ambalo linaumiliki wa vitalu vya
maili 25 huko Ilogelo wilaya ya Uvinza.
Pamoja na hilo pia anamiliki Kampuni ya Gombe Advisors
ambayo inahisa asilimia 25 katika Kampuni ya Leka Dutigite.
Zaidi ameeleza kuwa ameanza kuchangia mfuko wa Hifadhi za
Jamii(NSSF), tangu mwaka 2004.
Mbali na hilo la ukwasi, Zitto alieleza bayana juu ya
madeni aliyoyakopa kwa nyakati tofauti wakati akiwa mbunge, ambayo yana jumla
ya Sh. milioni 174.6.
Kwa nyakati tofauti, Zitto amekuwa akihusishwa na kuwa na
ukwasi wa hali ya juu yakiwamo magari ya kifahari jambo ambalo amekuwa
akilikanusha.
Mwaka 2012 alikaririwa na vyombo vya habari pasipo kutaja
thamani, alisema kuwa anamiliki nyumba yenye vyumba viwili huko Kigoma.
“Sijawahi kuwa na nyumba wala kiwanja hapa Dar wala
Dodoma isipokuwa nyumbani Kigoma, huko nina nyumba ya vyumba viwili tu ambayo
niliijenga wakati wa uchaguzi baada ya wazee kunishauri kuwa siyo vizuri
kuendelea kutumia nyumba ya baba yangu…Nina akaunti mbili tu moja benki ya NMB
na nyingine benki ya CRDB na zote hazina fedha zaidi ya shs Mil. 15 kila moja.”
Alikaririwa wakati huo.
Pia alitoa utetezi wake wa umiliki wa magari, ambapo
alisema kuwa anamiliki gari aina aina ya Land Lover, Free Lander pamoja na gari
dogo aina ya Toyota Vista.
“Baada ya kuwa mbunge , nakumbuka April 2007 niliingiza
nchini gari aina ya Hammer na nadhani nilikuwa mtu wa pili kuingiza gari hilo
hapa nchini, Kaka yangu Salum anayefanya biashara ya magari ndiye aliyeniletea
na hili sikuliendesha zaidi ya wiki mbili, likanishinda. Lilikuwa la kifahari
mno, nikamwambia alichukue aliuze na hela yangu anirudishie,” alikaririwa
Zitto.
No comments:
Post a Comment