OFISA Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na
Udhamini (RITA), Philip Saliboko, amesimamishwa kazi.
Hatua hiyo inatokana na kesi inayomkabili katika Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu inayohusu kupokea mgawo wa fedha kutoka Akaunti ya
Tegeta Escrow.
Kwa mujibu wa taarifa iliopatikana jana na kuthibitishwa
na Saliboko mwenyewe, kusimamishwa kwake ni kutokana na sheria za utumishi wa
umma.
Sheria ya utumishi wa umma inamtaka mtumishi yeyote
anapokabiliwa na kesi kusimamishwa akisubiri hatima ya suala lake.
Taarifa hiyo ilieleza kwamba nafasi ya Saliboko inachukuliwa na Emmy
Hudson ambaye anakuwa Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa RITA.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
ilimfikisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Saliboko kwa tuhuma za
kupokea rushwa.
Wakati kesi hiyo ikifikishwa, Mwendesha Mashtaka wa
TAKUKURU, Denis Lekayo, alidai Saliboko anatuhumiwa kupokea rushwa ya sh.
milioni 40.4, kutoka kwa mfanyabiashara James Rugemalila.
Kwa mujibu wa Lekayo, fedha hizo ni sehemu ya zilizokuwa
fedha za katika Akaunti Escrow na kwamba Saliboko alipokea fedha hizo kupitia
akaunti yake iliyokuwa katika Benki ya Mkombozi.
Saliboko aliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti
ya dhamana ambayo ni pamoja na kuwa na wadhamini wawili ambao kila mmoja
alitakiwa awe na fedha taslimu sh. milioni 22.
UHURU ONLINE
No comments:
Post a Comment